Uncategorized

Hamnitishi na ICC, asema Murkomen

Na BENSON MATHEKA August 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen, jana aliwajibu vikali wale aliotaja kama watu wanaojaribu kuwatisha maafisa wa polisi kwa madai kwamba wamehusika na uhalifu dhidi ya Wakenya wakitekeleza majukumu yao ya kazi.

Waziri huyo alisema kuwa hataogopa “wanaopenda vurugu wanaowatisha Wakenya wasio na hatia na sasa wanajificha nyuma ya madai kwamba hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahalifu ni sawa na uhalifu unaofaa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).”

“Sitaogopa vitisho vya ICC. Watisheni wengine, si watu wanaojua sheria,” alisema Murkomen, ambaye aliahidi kuwatetea maafisa wa polisi ili wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria bila hofu wala upendeleo.

Akizungumzia kesi iliyowasilishwa mahakamani na mwanasiasa Reuben Kagame dhidi yake, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohammed Amin kuhusiana na jinsi maandamano ya hivi majuzi yalivyoshughulikiwa, Murkomen alisisitiza kuwa anaamini kikamilifu kuwa walitenda kwa mujibu wa sheria.

Mnamo Alhamisi mwimbaji wa nyimbo za Mungu Reuben Kigame aliwasilisha kesi mahakamani akitaka kuwashtaki wakuu wa usalama kama watu binafsi  na Murkomen kwa mauaji ya vijana wakati wa maandamano ya Gen Z mwaka jana na mwaka huu.

Msingi wa kesi ya Bw Kigame ni kwamba  Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Igonga alifeli kuwashtaki polisi waliohusika na mauaji ilhali kuna ushahidi wa kutosha unaowahusisha na dhuluma na mauaji.

Bw Kigame anataka washtakiwe kwa mauaji ya kiholela, utekaji nyara, unyanyasaji na mauaji ya raia waliokuwa wakisaka haki.
Sehemu ya ushahidi wake katika kuwaandama wakuu hao kupitia mashtaka ya kibinafsi ni ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNHCR) mnamo Julai 2024.

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa kwenye maandamano ya mwaka jana, zaidi ya watu 39 waliuawa na wengine 39 wakatekwa nyara.
Anadai kuwa wakati wa maandamano ya Gen Z kwa miaka hiyo miwili, uhalifu ulitekelezwa na maafisa hao wa serikali na kuchangia mauti ya watu 91 huku wengine wakihepa.

Jana, Bw Murkomen alisema polisi hawakufanya makosa.

“Ningependa kusema kuwa nina uhakika na niko wazi kabisa kuwa Inspekta  Mkuu wa polisi na timu yake walifanya kazi kwa bidii na ndani ya mipaka ya Katiba kutetea taifa hili. Tukipewa nafasi tena, tutafanya vivyo hivyo kama wizara inayohusika na masuala ya usalama,” alisema Murkomen.

Alieleza kuwa usalama si jambo la kuchezewa na hakuna nafasi ya majaribio kwa wale wanaotaka kuingiza siasa katika suala hilo.

“Hatuna muda wa kufanya majaribio ya kisiasa kuhusu nani atapelekwa kortini na nani. Tunajua sheria. Mimi mwenyewe ni wakili na si hayo tu, nimefunza sheria,” aliongeza.

Bw Murkomen alisema anafahamu vyema Mkataba wa Roma, Kanuni ya Adhabu na sheria nyingine husika, na hivyo DCI au maafisa wengine waliotajwa kwa uovu kwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria kuhakikisha usalama wa nchi, watatetewa kwa nguvu zote.

Aidha, aliwakosoa vikali wanaolenga maafisa wa polisi ilhali hawakemei wale waliohusika kuchoma vituo vya polisi, magari ya serikali, ofisi za utawala na hata washukiwa waliokuwa wakishikiliwa katika kituo cha polisi cha Ol Kalau.

Akihutubia wanahabari katika Kaunti ya Kajiado, Waziri huyo alisisitiza dhamira yake ya kulinda maisha ya Wakenya, mali yao na taifa kwa ujumla dhidi ya “wanaopenda vurugu wanaolenga kusababisha fujo na uharibifu kwa kuvuruga utawala wa kikatiba.”