Wetang’ula ataka Magharibi waunge Ruto wakiotea urais 2032
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, amewataka wakazi wa eneo la magharibi kumuunga mkono Rais William Ruto akisema hatua hiyo itapatia jamii hiyo nafasi nzuri zaidi ya kutoa rais wa Kenya ifikapo mwaka wa 2032.
Akihutubu Ijumaa wakati wa maadhimisho ya miaka miwili ya Western Women Congress katika Shule ya Sekondari ya Busibwabo, Kaunti ya Busia, Wetang’ula alisema kuna nafasi kubwa ya eneo hilo kutoa rais wa sita wa Kenya baada ya utawala wa Rais Ruto.
“Sisi tuna nafasi bora ya kumrithi Rais Dkt William Ruto mwaka wa 2032,” alisema Wetang’ula. “Kwa hivyo nawahimiza tuunge mkono juhudi zake za kuchaguliwa tena mwaka wa 2027 ili kufanikisha ndoto hii.”
Spika huyo alieleza kuwa Rais Ruto tayari ameonyesha nia njema kwa eneo la Magharibi kwa kumteua Musalia Mudavadi kuwa Mkuu wa Mawaziri pamoja na viongozi wengine kutoka eneo hilo katika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Wetang’ula alisisitiza kuwa umoja wa kisiasa hautaimarisha uwezo wa jamii ya hilo kujadiliana kisiasa, bali pia unaweza kumshawishi Rais kuikabidhi jamii hiyo uongozi wa nchi.
“Umoja wetu na kumuunga mkono Rais kupata muhula wa pili kunaweza kumtia moyo kufikiria kumpa mmoja wetu usukani wa taifa hili,” alieleza.
Spika pia alikaribisha uamuzi wa hivi majuzi wa chama cha ODM kushirikiana na serikali ya Rais Ruto, akisema hatua hiyo imesaidia kupunguza joto la kisiasa na kuleta utulivu nchini.
Wetang’ula alipongeza Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kwa kuweka kando matamanio yake ya kisiasa na kushirikiana na serikali, akisema viongozi wengine wenye ndoto za urais wanapaswa kuiga mfano huo kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.
Aidha, Spika aliwataka viongozi wa upinzani kumpa Rais muda wa kutekeleza majukumu yake, akisema njama ya kuchochea maandamano na vurugu haifai kwa taifa.
“Wakosoaji wa Rais wanamhukumu kwa ukali mno, kwa muda mfupi ambao amekuwa madarakani amefanya vizuri sana na anahitaji muda kutimiza ahadi zake,” alisema Wetang’ula.
Aliongeza kuwa Rais Ruto yuko karibu kuifanya Kenya kuwa taifa lenye utoshelevu wa chakula kupitia mpango wa ruzuku kwa pembejeo za kilimo.