Habari za Kitaifa

Maraga aahidi kuzima ufisadi akipata urais

Na  George Munene August 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAJI Mkuu mstaafu David Maraga ameahidi kuangamiza janga la ufisadi iwapo atachaguliwa Rais 2027.

Akihutubia wanachama wa chama cha United Green Movement (UGM) katika ukumbi wa Kanisa Katoliki la Holy Rosary mjini Kutus, alipozuru Kaunti ya Kirinyaga, Bw Maraga alilalama kuhusu uporaji wa fedha za umma uliokithiri huku akiahidi kuukomesha kabisa.

Bw Maraga alisisitiza kuwa ana uwezo wa kutosha kulinda mali ya umma na akawataka Wakenya wamwamini. “Ninawania urais na nawaomba Wakenya waniamini, nitapambana na ufisadi hadi mwisho,” alisema.

Bw Maraga alisema aligundua hali si nzuri nchini baada ya kizazi cha Gen Z kuvamia Bunge kupinga hali ya uchumi. “Maisha yamekuwa magumu kwa kila mmoja kwa sababu ya ufisadi, na ndio maana Gen Z walivamia Bunge kuonyesha hasira zao. Nakubaliana nao kuwa tatizo kuu la nchi hii ni ufisadi. Nikichukua uongozi, nitaiweka Kenya katika njia bora,” alisema.

Alieleza kuwa rasilimali za nchi zikisimamiwa vyema, kila Mkenya atafaidi na kuboresha maisha. “Viongozi walioko sasa wanaiba mali ya umma, ndio sababu hakuna dawa hospitalini na hakuna fedha za kufadhili elimu,” aliongeza.

Aliahidi kutekeleza Katiba kikamilifu ili kufanikisha vita dhidi ya ufisadi, ambao amesema umewaacha Wakenya wengi katika hali ya umaskini.Bw Maraga aliwasihi Wakenya wampigie kura kwa wingi ili aweze kumng’oa Rais William Ruto, ambaye alidai kuwa uongozi wake hauruhusu maendeleo.

“Tushirikiane na kuiondoa serikali hii kupitia kura. Tumechoka na ufisadi unaoathiri kila sekta ya uchumi,” alisema.Aidha, Bw Maraga alieleza kuwa uchumi wa nchi umeharibika kwa sababu ya uongozi mbovu na akaongeza kuwa ana uwezo wa kuuimarisha.

“Uchumi wetu umeanguka, na nina suluhisho la kuurekebisha kwa manufaa ya kila Mkenya,” alisema.Alikashifu serikali ya Kenya Kwanza kwa mpango wa kuagiza mchele wa bei nafuu bila ushuru kutoka nje ya nchi.

Alisema ni jambo la kushangaza kuwa serikali inapanga kuagiza mchele kutoka nje ilhali mchele wa wakulima wa Mwea unaoza kwenye maghala. “Serikali hii haijali wananchi wake. Inavutiwa tu na kunufaisha mataifa mengine kwa hasara ya wakulima wetu. Serikali hii iondolewe kwa kura,” alisisitiza.

Alisema wakulima wa mchele ni watu muhimu na wanapaswa kulindwa ili wapate soko la bidhaa zao. “Huo mchele utaagizwa na mabwanyenye kwa gharama ya wakulima wetu. Huu ni ufisadi na hatutaruhusu,” aliongeza.

Akiandamana na mwaniaji wa nafasi ya Mwakilishi wa Kike Kirinyaga, Bi Emma Waithira, Bw Maraga aliwahimiza Wakenya kuungana naye katika kushinikiza mabadiliko ya uongozi bila kuogopa.

Wakati huohuo, alimkosoa Rais Ruto kwa kutoa amri kwa maafisa wa usalama kuwafyatulia risasi miguuni wale wanaovamia vituo vya polisi au miundombinu ya serikali.

Alisema amri hiyo ni ukiukaji wa Katiba akiongeza kuwa washukiwa wanapaswa kukamatwa, kushtakiwa na kuhukumiwa iwapo watapatikana na hatia na si kuuawa.“Hii ni mara ya kwanza kumsikia Rais akitoa amri isiyo ya kikatiba. Washukiwa wanapaswa kushtakiwa sio kupigwa risasi,” alisema.

TAFSIRI: BENSON MATHEKA