Wakulima wa miwa kutimiza masharti magumu ya mikopo ili kudhibiti madeni
Wakulima wa miwa wanaonuia kupata mkopo kutoka kwa Hazina ya Maendeleo ya Miwa (SDF) wanakabiliwa na masharti magumu zaidi, huku serikali ikichukua hatua kuzuia ongezeko la waliokosa kulipa mikopo ambayo imefikia mabilioni ya shilingi.
Katika mpango mpya wa kuwaondoa wakopaji sugu wa mikopo, serikali imepatia kipaumbele historia ya mikopo ya wakulima, ikiwa ni pamoja na hitaji la kuwasilisha cheti kutoka kwa Shirika la Kutathmini Mikopo (CRB) na Ushuru wa Mapato kutoka Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA).
‘Ili kufuzu kwa mkopo wa SDF, mwombaji atalazimika: a) kufuata kanuni, miongozo na viwango vya sekta; b) asiwe na mkopo anaoendelea kulipa kutoka kwa bodi; c) kuwasilisha fomu ya maombi iliyojazwa kikamilifu pamoja na pendekezo la biashara; d) kuwasilisha nakala ya Cheti cha PIN cha KRA; e) kuwasilisha Cheti halali cha Uzingatiaji wa Ushuru; f) kuwasilisha Fomu halali ya CR12; na g) kuwasilisha ripoti ya CRB,’ serikali ilisema.
Ulipaji wa mikopo chini ya SDF umekuwa changamoto kwa miaka mingi, huku wakopaji wakikosa kulipa kiasi kinachokadiriwa kuwa Sh3.7 bilioni kufikia mwaka jana.
Katika juhudi za kuwakabili “wakulima hewa” wanaolenga fedha kutoka kwa hazina hiyo, serikali sasa inataka waombaji binafsi kuwasilisha nakala ya kitambulisho cha kitaifa, ramani ya eneo la mradi na iwapo wanatumia ardhi kama dhamana, watoe nakala ya hatimiliki ya ardhi, ramani za ilipo ardhi( GPS)
Hazina hii inasimamiwa na Bodi ya Sukari ya Kenya (KSB) na inafadhiliwa kupitia ushuru mpya wa Maendeleo ya Sukari (SDL) uliorejeshwa upya, unaokusanywa na KRA. SDL hutozwa kwa sukari ya ndani na ile ya kuagizwa kutoka nje.
Kila kiwanda cha kusindika sukari hulipa asilimia nne ya bei ya bidhaa katika kiwanda kufikia tarehe 10 ya mwezi unaofuata baada ya sukari kuzalishwa. SDL pia hulipwa kwa asilimia nne ya gharama ya CIF (gharama, bima na usafirishaji) ya kila shehena ya sukari inayoingizwa chini ya ushuru wa kawaida wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
CIF ni mkataba wa kimataifa wa usafirishaji ambao unajumuisha gharama zinazolipwa na muuzaji kufidia usafirishaji, bima na gharama nyingine hadi bidhaa zinapomfikia mnunuzi.
KRA ilianza kukusanya ushuru huu wa SDL Julai 1 2025, na mapato hayo yatatumika kufadhili KSB, Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Sukari Kenya (KESRETI), uthabiti wa bei kwa wakulima wa miwa, na maendeleo ya miundombinu ya sekta hiyo.
Asilimia 15 ya SDL ni kwa maendeleo na ukarabati wa viwanda, asilimia 15 kwa utafiti na mafunzo chini ya KESRETI, asilimia 40 kwa ukuzaji wa miwa na uzalishaji, asilimia 15 kwa maendeleo na ukarabati wa miundombinu katika maeneo yanayolima miwa, asilimia 10 kwa usimamizi wa KSB, na asilimia 5 kwa mashirika ya wakulima wa miwa.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA