Habari za Kitaifa

SRC yapinga Mswada wa kuongezea majaji marupurupu

Na  DAVID MWERE August 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TUME ya Mishahara (SRC) imepinga Mswada utakaowagharimu walipa ushuru zaidi ya Sh15 bilioni kuboresha marupurupu ya majaji wa mahakama kuu wakati huu taifa linakabiliwa na wakati mgumu kufadhili shughuli zake.

Serikali itagharamikia kikamilifu marupurupu hayo kwa sababu majaji wameepushiwa kuchangia kufadhili marupurupu yao licha ya SRC kupendekeza Mpango Maalum wa Mchango kuambatana na sera iliyopo ya serikali na kuainisha nyongeza ya malipo ya uzeeni na vipengee vya Sheria kuhusu Nyongeza ya Pesa za Kustaafu 2005.

SRC ambayo ni tume huru inasema kupitia notisi aliyotumiwa karani wa Bunge la Kitaifa, Samuel Njoroge, kwamba Mswada wa Marupurupu ya Kustaafu kwa Majaji 2025 uliowasilishwa bungeni una dosari na ni sharti urekebishwe.

Mswada huo unanuiwa kukabidhi Tume ya Huduma za Idara ya Mahakama (JSC) inayoajiri majaji mamlaka bila kipimo kutoa mapendekezo kuhusu marupurupu ya kustaafu kwa maafisa wa idara ya mahakama ikisaidiwa na SRC.

Hata hivyo, kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa SRC, Margaret Njoka, alifichua tume hiyo inatofautiana na mswada huo kwa sababu unakiuka kanuni za nchi kuhusu ustawishaji na unaingilia moja kwa moja wajibu wake kinyume cha katiba.

Bi Njoka alisema Mswada huo unakiuka Kifungu 230 (4) (a) cha katiba kuhusu wajibu wa SRC- ulivyofafanuliwa na Mahakama Kuu 2015.

Taarifa hiyo inasema marupurupu ya kusafiri na matibabu baada ya kustaafu yaliyopendekezwa katika Mswada huo yanayogharimu Sh1.74 bilioni kwa mwaka mmoja, hayajawekwa na SRC kuambatana na wajibu wake kikatiba.

“Pendekezo la kuwaongezea majaji wa mahakama kuu marupurupu ya kustaafu ni sawa na kuipokonya SRC majukumu yake kikatiba ya kuweka na kubadilisha mara kwa mara malipo na marupurupu ya maafisa wa umma, ikiwemo marupurupu ya kustaafu,” alisema Bi Njoka.

Changamoto za kifedha zinazoandama taifa kutokana na deni kubwa na mapato kudorora zilisababisha Waziri wa Fedha John Mbadi kutangaza majuzi kupunguza mgao wa fedha za shule za sekondari kutoka Sh22,244 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka hadi Sh16,900.

TAFSIRI: MARY WANGARI