Sababu za Natembeya na Wamalwa kukoseshana usingizi chamani
Chama cha Democratic Action Party – Kenya (DAP-K) kimejikuta katika hali ya sintofahamu baada ya viongozi wake wawili mashuhuri, Kiongozi wa Chama Eugene Wamalwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, kutishiwa kuondolewa kutoka nyadhifa zao muhimu.
Makundi pinzani yamekuwa yakipanga njama za kudhoofisha ushawishi wa viongozi hao kwa kuwatuhumu kwa kutokuwa waaminifu au kuvuka mipaka katika masuala ya chama. Migawanyiko hii imefichua tofauti kubwa ndani ya chama, jambo linalozua hofu kuhusu mshikamano wake kuelekea chaguzi zijazo.
Kufuatia ripoti za mgawanyiko, uongozi wa DAP-K umeamua kuwasilisha masuala yote kwa Kamati ya Utatuzi wa Mizozo ya Ndani ya Chama.
Inaripotiwa kuwa Gavana Natembeya, ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama, anaongoza kundi linalotaka chama kirekebishwe ili kivutie kitaifa, huku Bw Wamalwa akiongoza upande wa kihafidhina unaopendelea kudumisha muundo na mwelekeo wa sasa wa chama.
Akihutubia wanahabari Ijumaa, Katibu Mkuu wa DAP-K Dkt Eseli Simiyu alikiri hali ya mgogoro mkubwa akisema: “Kuna mgogoro mkubwa miongoni mwa wanachama wa chama.” Alieleza kuwa Kamati ya Utatuzi wa Mizozo ya Ndani itatatua masuala yote na kuelekeza hatua itakayofuata kwa chama.
“Kufuatia mashaka yaliyojitokeza kuhusu uhalali wa baadhi ya wanachama wa Kamati ya Utendaji ya Kitaifa (NEC), ombi la kumwondoa kiongozi wa chama na maafisa wengine wa NEC, pamoja na Naibu Kiongozi wa Tatu wa Chama, limejadiliwa na Baraza Kuu la Usimamizi (NMC) na kubaini kuwa kuna mgogoro mkubwa wa wanachama,” alisema Dkt Simiyu.
Aliongeza kuwa NMC imeamua kuwasilisha malalamishi yote kwa mfumo wa ndani wa kutatua mizozo (IDRM) kwa haraka ili kuhakikisha shughuli za chama – hususan uchaguzi mdogo ujao – zinaendelea bila kukwama.
Kwa upande wake, Bw Wamalwa aliwataka wanachama wa chama kuwa watulivu akiwahakikishia kuwa mizozo hiyo itatatuliwa kwa njia ya kidemokrasia. Alithibitisha kuwa chama kitawasilisha wagombea kwenye chaguzi ndogo zijazo katika maeneo ya Malava na Ugunja.
“Sihisi kutishwa kwa vyovyote; hiki ni chama cha kidemokrasia. Hakuna jambo ambalo hatuwezi kushughulikia,” alisema Bw Wamalwa.
Bw Wamalwa, ambaye ni mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani nchini Kenya, anasemekana kukumbwa na upinzani kutoka kwa kundi linalohisi uongozi wake kuwa wa kiimla na usiohusisha wengine. Baadhi ya wanachama wa chama wanamtuhumu kwa kufanya maamuzi ya kibinafsi bila mashauriano ya kutosha, jambo ambalo linawavunja moyo wafuasi wa mashinani.
Kwa upande wake, Gavana Natembeya alikanusha madai ya kuwepo kwa mizozo ndani ya chama, akisema ni tofauti ndogo tu. Alihimiza mabadiliko ndani ya DAP-K na kutaka chama kijitanue zaidi ya eneo la Magharibi mwa Kenya.
“Minong’ono mnaosikia ndani ya DAP-K ni kati ya wahafidhina na wale wanaotaka mageuzi – wanaotaka chama kirekebishwe kiwe cha kitaifa, si cha Magharibi tu. Siasa si za Magharibi pekee,” alisema.
“Hapo ndipo changamoto ipo. Wapo wanaopinga kufungua mlango kwa Wakenya wengine kusaidia DAP-K kukua, ilhali tunajua kina uwezo mkubwa,” aliongeza.
Kauli ya gavana huyo ilijiri baada ya ombi la kumwondoa kuwasilishwa Alhamisi, Julai 31, akilaumiwa kwa kufadhili na kuendeleza chama kingine cha kisiasa – Conservation for Democracy in Kenya (COD-K) – kwa kutumia vibaraka.
Sehemu ya ombi hilo linasema: “Ombi la kumfukuza Naibu Kiongozi wa Chama na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, kwa kufadhili usajili na/au uendelezaji wa chama kingine cha kisiasa kiitwacho Conservation for Democracy in Kenya (COD-K) kwa kutumia mawakala.”
Alhamisi, kundi la wabunge wa DAP-K lilikemea vikali wakosoaji wa uongozi wa chama na wale wanaojaribu kuudhoofisha. Walionyesha wasiwasi kuhusu ripoti ya mpango wa pamoja wa kupindua uongozi wa chama kwa njia isiyo ya kikatiba.
Chama kilidai kuwa mpango huo unashinikizwa na nguvu za nje kupitia mmoja wa viongozi wake ambaye anajifanya kuwa mtetezi wa demokrasia na watu wa Magharibi, lakini kwa kweli anatenda kinyume.
Wabunge hao walisisitiza kuwa kiongozi huyo amekuwa akifurahia uungwaji mkono wa kisiasa, kimaadili na wa kisheria kutoka kwa uongozi wa chama.
“Juhudi zozote za kupindua uongozi wa DAP-K kwa njia isiyohalali, zenye kulenga kumwondoa Kiongozi wa Chama Eugene Wamalwa na viongozi wa kitaifa, zitakabiliwa na upinzani mkali. Tumejulishwa kuhusu chama chake kipya na tunamtahadharisha dhidi ya njama za kudhoofisha DAP-K anapoondoka,” ilisema taarifa hiyo.
Kundi la wabunge wa DAP-K liliweka bayana kuwa lina imani kamili kwa Kiongozi wao Bw Wamalwa. Walisema anastahili kuungwa mkono na viongozi wote wa chama na wafuasi wake badala ya kuhujumiwa, hasa wakati huu muhimu ambapo chama kimeelekeza juhudi zake katika masuala ya maendeleo yanayolenga kuinua maisha ya Wakenya.
“DAP-K si tu chama cha tano kwa ukubwa nchini Kenya, pia ni mojawapo ya vyama thabiti na vilivyo mstari wa mbele katika kupambana na ufisadi, ukosefu wa haki kijamii, ukiukaji wa haki za binadamu, na utetezi wa katiba,” walisema.
“Tunaendelea kushikilia kwa dhati maadili haya msingi na kulinda mfumo wa vyama vingi nchini Kenya.”
Chama hiki kilikuwa miongoni mwa vyama 23 vilivyoshiriki kwenye Uchaguzi Mkuu wa Kenya wa 2022 kama sehemu ya muungano wa Azimio La Umoja. Kati ya wagombeaji wake 61, ni watano pekee waliweza kuchaguliwa katika Bunge la 13 la Kenya.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA