Wahuni wakaidi amri ya mahakama kuhusu shule inayozozaniwa
LANGO la Shule ya Msingi ya Gatoto liliendelea kubaki limefungwa huku wahuni wakikaidi agizo la mahakama lililowataka warejeshe shule hiyo kwa jamii na kwa usimamizi wa awali chini ya Gideon Ndambuki.
Kutoka mbali, mwandishi wa Taifa Leo aliwaona watu waliokuwa ndani ya shule hiyo wakiwazuia wazazi na uongozi wa zamani kuingia.
Mvutano huo ulitokea baada ya uamuzi wa mahakama kuamuru shule hiyo, ambayo ilichukuliwa kwa nguvu na serikali kupitia Wizara ya Elimu na kubadilishwa kuwa shule ya umma, irejeshwe kwa usimamizi wa awali.
Wazazi waliounga mkono uamuzi wa mahakama walielezea masikitiko yao kuhusu ada kubwa wanazotozwa tangu serikali ichukue usimamizi wa shule hiyo.
Bi Pauline Akoth, mama wa watoto watatu wanaosoma Gatoto, alisema hali imekuwa ngumu kwao tangu serikali iingilie kati.
“Wanatwambia ni shule ya serikali, lakini ukihesabu ada tunayolipa sasa ni ya juu kuliko hapo awali. Shida tuliyonayo sasa ni kuhusu pesa za safari za shule tunatakiwa kulipa Sh4,000, mitihani Sh2,000. Hadi sasa watoto wetu wengi walibaki nyumbani, hawakufanya mitihani,” alieleza Akoth.
Awali, wazazi walikuwa wakilipa Sh2,750 kwa muhula wa kwanza fedha hizo zilihusisha chakula, mitihani, karo na masomo ya ziada. Kwa muhula wa pili, walilipa Sh1,500 na Sh1,000 kwa muhula wa tatu.
Wazazi pia walidai shule hiyo imebadilika kabisa, hali iliyowalazimu kuanza kutafuta shule mbadala kwa watoto wao. Virginia Wanjiru alisema uongozi wa sasa hauelewi hali yao ya kiuchumi kwani wanatoka mitaa ya mabanda.
“Nilienda kuomba barua ya kuhama shule lakini nikaambiwa nilipie Sh9,000. Nilishangaa, nilihitaji tu barua ya kuhamisha mtoto,” alisema Wanjiru.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi, Bw Felix Mwangangi, alisema baada ya kushinda kesi mahakamani, walirejea kutekeleza agizo hilo la mahakama.
“Tangu shule ichukuliwe, tumekuwa na matatizo mengi. Kuna ada nyingi zisizo na maelezo, watoto wanalazimishwa kwenda masomo ya ziada. Ikitokea Ijumaa na mtoto hajalipa karo hiyo ya ziada, anarejeshwa nyumbani jambo ambalo si haki,” alisema Bw Mwangangi.
Meneja wa Mradi wa Maendeleo Jumuishi wa Gatoto, Bw Gideon Ndambuki, ambaye pia ni mkurugenzi, alisema mahakama iliagiza warudishiwe usimamizi wa shule hiyo kufikia Juni 12. Hata hivyo, alidai wanasiasa wa eneo hilo wamekuwa wakiwatuma wahuni wakisaidiwa na polisi kuwazuia kuingia shuleni.
“Mahakama Kuu ya Milimani ilitoa uamuzi kwa niaba yetu. Jaji Bahati Mwamuye aliamuru kuwa mshtakiwa wa tano, aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa PTA, ajiondoe kabisa katika shughuli zote za Gatoto. Pia iliamuriwa kuwa uongozi uliokuwepo kwa zaidi ya miaka 25 urejeshwe. Lakini leo tumekuja, tumekuta lango limefungwa na tukaambiwa haturuhusiwi kuingia,” alisema Bw Ndambuki.
Hata hivyo, Msaidizi binafsi wa Mbunge Julius Mawathe, Bw Urbanus Musau, aliyekuwepo eneo hilo, alisema shule hiyo tayari iko chini ya Wizara ya Elimu, ina hatimiliki, na inatambulika kama shule ya umma.
“Shule hiyo ilinyakuliwa na NGO inayojitambulisha kama jamii. Ingawa mahakama iliagiza warejeshe, tulikata rufaa mara moja, na kesi hiyo itaanza kusikizwa Agosti 6. Tayari tuliwatumikia stakabadhi za mahakama, kwa hivyo tunashangaa kwanini wanarudi kuichukua shule kabla ya kesi kusikilizwa,” alisema Bw Musau.
Musau alidai kuwa shule hiyo ilikuwa na jumla ya wanafunzi 800 hapo awali, lakini sasa ina wanafunzi zaidi ya 4,000 huku ikiwa na mwalimu mkuu mmoja na naibu wawili pekee.
Kwa upande wake, Bw Ndambuki alikanusha kupokea barua rasmi ya rufaa kutoka kwa upande wa pili akisema walipokea tu notisi ya nia ya kukata rufaa.
“Nimeambiwa kuwa wapinzani wetu hawajakata rufaa rasmi mahakamani. Walichotoa ni notisi tu ya nia ya kukata rufaa ambayo haimaanishi kuwa rufaa hiyo imewasilishwa,” alisema Bw Ndambuki.