Naomba radhi kwa kuunga serikali ya uongo, asema mwandani wa Ruto akihamia kwa Kalonzo
MWANDANI mkuu wa Rais William Ruto kutoka eneo la Ukambani James Mbaluka amemwasi na kuamua kushirikiana na kambi ya Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.
Bw Mbaluka, ambaye Rais Ruto alikuwa amemteua kuwa Waziri Msaidizi wa Afya (CAS) kabla ya mahakama kuzima hatua hiyo, amemsuta kiongozi wa taifa “kwa kusimamia nchi vibaya na kushindwa kuimarisha maisha ya Wakenya”.
“Ni makosa kwa Rais kutoa ahadi kochokocho wakati wa kampeni na kufanya kinyume kabisa na alivyoahidi.
“Niliongoza kampeni ya Rais Ruto katika Kaunti ya Makueni. Tuliahidi kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi lakini sasa imebainika kuwa tuliwahadaa. Leo hali ni mbaya zaidi kwa makundi ya vijana na wanawake chini ya utawala huu wa Rais Ruto,” Bw Mbaluka akasema akiwa katika kijiji cha Makutano, Kaunti ya Makueni, Jumamosi.
Mgombeaji huyo wa kiti cha eneobunge la Kibwezi Magharibi kwa tiketi yaa chama cha UDA mnamo 2022 alisema hayo wakati wa mazishi ya Garshon Mutisya Mwove, aliyepigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya Juni 25 mjini Emali, Kaunti ya Makueni.
Marehemu Mwove aliyekufa akiwa na umri wa miaka 33, amemwacha mjane na mtoto mmoja mvulana. Bw Mbaluka, ambaye pia ni mfanyabiashara aliomba msamaha kwa waombolezaji kwa kuwa miongoni mwa watu waliompigia debe Rais Ruto katika kaunti hiyo.
“Ni uchungu kuhadaa wapigakura. Ningependa kuanza kwa kuwaomba msamaha,” akasema huku akishangiliwa na waombolezaji.
Walimshtumu Rais Ruto kwa kuendeleza utekaji nyara, mateso na mauaji ya waandamanaji waliokuwa wakipinga utawala wake.
Bw Mbaluka alipuuzilia mbali michango ya kuyapiga jeki makundi ya vijana na akinamama inayoongozwa na Naibu wa Rais, Prof Kithure Kindiki, akiyataja kama kinyume na mpango wa kuwainua wasiojiweza kiuchumi.
Rais Ruto alipozuru Makueni kuhudhuria ibada ya kanisa mwaka mmoja uliopita, Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka alimwomba awateue serikalini Bw Mbaluka na aliyekuwa Mbunge wa Machakos Mjini Victor Munyaka.
Lakini kiongozi wa taifa alipuuzilia mbali pendekezo hilo akisema haja yake kuu wakati huu ni kuzalisha nafasi za ajira kwa mamilioni ya vijana kote nchini.