Habari

Kabarak yakana kunyima vitukuu wa Moi nafasi shuleni

Na JOSEPH OPENDA August 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

USIMAMIZI wa Shule za Kabarak umekanusha kuwa ulikataa kuruhusu vitukuu wawili wa Rais Mstaafu Daniel arap Moi wajiunge na Shule ya Msingi ya Moi Junior na kuenda kinyume na amri ya korti.

Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kabarak, Prof Henry Kiplagat ambaye pia ni katibu wa Wakfu wa Chuo Kikuu cha Kabarak, alitetea taasisi hiyo kuwa ilipuuza amri ya korti kwa kukataa vitukuu hao wawili wajiunge na shule ya Moi Junior.

Akiwa mbele ya Hakimu Mwandamizi Kipkurui Kibelion baada ya kuagizwa afike kortini, alipuuza madai hayo na kusema Shule ya Moi Junior haikuwa imepokea barua kutoka kwa wazazi wa mtoto huyo ya kutaka kusomea shuleni humo.

Alisisitiza kuwa kuna mchakato wa kufuatwa katika kujiunga na shule hiyo na wa kwanza ni kujaza na kuwasilisha fomu za kutuma maombi.

“Hatujapuuza amri ya korti na hakuna maombi au ombi lolote ambalo limetumwa kwa mpango wowote wa masomo. Shule ya Msingi ya Moi Junior haijapata ombi lolote,” akasema.

Pia naibu chansela huyo alisema kuwa shule hiyo haipendelei au kutoa huduma bora kwa mwanafamilia yeyote ya Rais Moi akisema kuwa maombi yote lazima yafuate mchakato uliowekwa.

Prof Kiplagat alikuwa ameagizwa kwa nini hajafuata amri ya korti na kuruhusu watoto hao wajiunge na shule ya Moi Junior.

Hii ni kufuatia madai ya Collins Kibet, mjukuu wa Moi kupitia mawakili wake kuwa alikuwa akipata ugumu kuhakikisha wanawe hao wanajiunga na shule hiyo.

Mnamo Februari, mahakama iliamrisha Bw Kibet ahakikishe watoto wake wawili wanajiunga na mojawapo ya shule zinazosimamiwa na Kabarak na pia awajumuishe kwenye mpango wa bima ya matibabu.

Kwa kukosa kutimiza amri hii, Bw Kibet alizuiliwa kwa wiki mbili kuanzia Julai 9 kabla ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni.

Ijumaa iliyopita, Bw Kibet aliamrishwa aanze mchakato wa kuhakikisha kuwa watoto hao wanajiunga na shule ya Kabarak. Fomu hizo ziliwasilishwa na Prof Kiplagat kortini.

Bw Kibet amekuwa kwenye mvutano na aliyekuwa mkewe Gladys Jeruto Tagi ambaye amemshutumu kwa kukosa kujukumikia malezi ya watoto wao wawili.

Bi Jeruto aliwasilisha kesi akitaka Bw Kibet aadhibiwe kwa kupuuza amri ya korti 2022.

Amri hiyo ilimtaka agharimie elimu ya watoto hao, gharama ya matibabu na pia sehemu ya buradani, pesa zote zikiwa Sh1.5 milioni kwa mwaka. Alidai Bw Kibet alikuwa amefeli kutekeleza majukumu hayo na kumwacha na mzigo wa kutimiza maslahi ya watoto hao.