Mwanahabari wa NTV Trev alipenda magari akiwa mdogo, familia yasema ikimuomboleza
MWANAHABARI wa runinga ya NTV Trevor Lamenya maarufu kama Big Boy Trev aliyeaga dunia Jumamosi, ametajwa kama mtu mwenye maadili, mtulivu ambaye alikuwa anayapenda sana magari kuanza utotoni.
Bw Lamenya alikuwa akiendesha kipindi cha Cars With Big Boy Trev kwenye NTV.
Mnamo Jumapili, familia yake ilikongamana nyumbani kwake Nyayo Estate ambako babake George Lamenya alifichua kuwa marehemu alianza kuyapenda magari mapema miaka 90 akiwa darasa la pili.
Bw George alifichua kuwa aliponunua gari lake la kwanza, mwanawe alihiari kulala ndani siku ya kwanza.
Mwanahabari huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 40 na kipindi chake NTV ndicho kilikuwa kikiangazia magari pekee kati ya runinga zote nchini.
Kwa mujibu wa familia yake, Bw Trev alikuwa mnyonge Jumamosi ndipo akamuuliza babake amwache apumzike.
Alilemewa kupanda vidato vya kufikia nyumba yake na alikufa kwenye nyumba ya jirani.
Marafiki wengi wa Bw Trev akiwemo Ezra Chibole ambaye wamekuwa karibu naye kwa zaidi ya miaka 20, alisema mauti yake yamemshangaza sana.