Kigame adai kutafutwa na KRA siku mbili baada ya kushtaki wakuu wa usalama kwa mauaji
SIKU mbili baada ya msanii maarufu wa nyimbo za injili Reuben Kigame kuwasilisha kesi katika Mahakama Kuu dhidi ya wakuu wa usalama nchini kuhusiana na visa vya utekaji nyara na mauaji wakati wa maandamano ya Gen Z, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) inamtaka alipe malimbikizi ya ushuru wa Sh20 milioni.
Kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X (zamani, twitter) Bw Kagame anasema anaamini kuwa hatua hiyo sio sadfa bali KRA inatumiwa kumtisha na kumnyamazisha asikosea serikali.
“Alhamisi, Julai 31, 2025 nilipokea barua pepe kutoka kwa afisa mmoja wa KRA nitayemwita Bi DW akidai serikali inanidai ushuru wa kima cha Sh20 milioni. Hii ni licha ya kwamba mimi huchuma Sh200,000 kwa mwezi wakati biashara ni nzuri,” akasema.
“Ikizingatiwa kwamba kama mtu anayeishi na ulemavu (PLWD) ni haki yangu kupewa msamaha wa ushuru, lakini mimi hulipa ushuru kwa hiari,” Bw Kigame akaongeza.
Msanii huyo, ambaye mnamo 2022 alitangaza nia ya kuwania urais ila akafeli kuidhinishwa na tume ya uchaguzi, alifichua yeye ndiye anadai serikali mamilioni ya pesa kutokana na nyimbo zake za injili.
“Nitasema mengi baadaye, sitakubali kutishwa,” Bw Kigame akahitimisha taarifa yake.
Kupitia wakili wake Gitobu Imanyara, Bw Kigame, Alhamisi Julai 31, 2025 aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi akitaka aruhusiwa kuwashtaki Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen na Inspekta Jenerali Douglas Kanja.
Wengine anaopania kuwafungulia mashtaka ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) Noordin Haji na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor.
“Zaidi ya waandamanaji 100 waliuawa kiholela na maafisa wa serikali wakiwemo polisi kuanzia Juni 2024 hadi Juni 2025. Wengine wengi wametekwa nyara na kuteswa vibaya, lakini kiongozi wa mashtaka ya umma (DPP) Renson Ingonga amefeli kuwafungulia mashtaka wahusika,” Bw Kigame akaeleza.
Kulingana na msanii huyo, kesi yake ni hatua ya kwanza ya kualika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kulivalia njuga suala hilo.
“Maovu yaliyotekezwa na serikali dhidi ya raia yanasawiriwa kama uhalifu dhidi ya binadamu, unaopasa kushughulikiwa na mahakama ya ICC,” akaeleza.
Bw Kigame sasa anaingia kwenye orodha ya wakosoaji wa serikali ambao wameelekezewa vitisho kwamba wanadaiwa mamilioni ya fedha za KRA.
Mapema mwaka huu, mwanaharakati wa kisiasa Morara Kebaso, ambaye amekuwa akianika miradi ya serikali iliyokwama baada ya kufyonza mabilioni ya fedha za umma, alidaiwa Sh27 milioni kama malimbikizi ya ushuru.
Aidha, akaunti yake za benki zilifungwa na nambari yake ya siri (PIN) pamoja na cheti chake cha kuonyesha kuwa amekuwa akilipa ushuru kufutiliwa mbali na KRA.