Sifuna anaweza kupokonywa ukatibu wa ODM Oktoba, duru zasema
MATAMSHI ya Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kuwa hawezi kutia saini mkataba wowote utakaompa Rais William Ruto nafasi ya kuhudumu kwa zaidi ya muhula mmoja yamechemsha uongozi wa chama hicho huku duru zikiarifu huenda akapokonywa wadhifa wake chamani wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) hapo Oktoba.
Duru ziliarifu kuwa ODM inapanga kuandaa NDC katikati ya Oktoba ambapo wanachama wataamua mustakabali wa chama kuhusu uchaguzi wa 2027, urasmishaji wa uhusiano kati yao na Rais pamoja na kuwateua washikilizi wapya wa nyadhifa chamani.
Akiwa eneobunge la Saboti, Jumapili, Bw Sifuna alisema hawezi kulazimishwa kutia saini mkataba wowote wa kuunga Rais Ruto na iwapo hali itakuwa hivyo basi ataondoka ODM.
“Ninashikilia msimamo wangu na ningependa kuwaambia wale mabroka wa ODM kuwa nina haki ya kutoa maoni yangu. Nitakuwa nasoma maafikiano ya chama isipokuwa yale ambayo chama kitasema kuwa kitamuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027,” akasema Bw Sifuna.
“Niko tayari kuondolewa kama katibu mkuu wa ODM kwa sababu nimeambiwa tayari kuna mtu ambaye ameidhinishwa achukue nafasi yangu,” akaongeza.
Kauli yake iliungwa mkono na Mbunge wa Saboti, Bw Caleb Amisi ambaye pia alisema kuwa wako tayari kuondoka ODM kama chama kitamuunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili.
Pia Bw Sifuna alitangaza kuanzisha vuguvugu la Kenya Moja ambalo linashirikisha wabunge chipukizi kutoka mirengo yote ya kisiasa.
Taifa Leo imebaini kuwa wandani wa Bw Raila sasa wanapanga kutumia NDC ya Oktoba kumwondoa Bw Sifuna wakisema ana kiburi kingi na anatumiwa kuyumbisha chama akiwa ndani kisha kumwaibisha Raila.
“Sifuna aliongea vibaya Trans Nzoia kwa sababu anajua mambo yake chamani yameisha na hawezi kuhudumu kama katibu mkuu wa chama tena. Oktoba si mbali kwa sababu tutatumia mkutano huo kumfurusha kabisa, hata asithubutu kutetea wadhifa wake,” akasema mbunge mmoja wa ODM mwandani wa Bw Raila aliyeomba kutotajwa.
Tayari joto kuhusu kongamano hilo limeanza huku tofauti kubwa zikizuka kati ya wabunge wa ODM kutoka eneo la Magharibi na wenzao wa Nyanza kuhusu mienendo ya Bw Sifuna.
Wanasiasa wa ODM kutoka Magharibi wanaunga Bw Sifuna wakisema utawala wa sasa haujawanufaisha wakazi wao na hata baada ya Bw Raila kuingia serikalini, eneo hilo halijanufaika kama Nyanza kwa miradi ya maendeleo.
“Anapotumia neno broka alikuwa akimlenga nani? Aliogopa kuwasema kwa nini? Sifuna hatahudumu kama katibu mkuu wa ODM kuanzia Oktoba,” akaongeza mbunge huyo.
Bw Sifuna amekuwa katibu mkuu wa ODM tangu Februari 2018 alipochukua wadhifa huo kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Budalang’i Ababu Namwamba aliyekuwa amegura chama kuelekea uchaguzi wa 2017 na kuunga Jubilee.
Wiki jana, Bw Odinga aliandaa mkutano wa ngazi ya juu chamani ambapo iliafikiwa kuwa msimamo wa ODM kuhusu masuala mbalimbali utakuwa ukifahamishwa umma kupitia ngazi mbalimbali za chama.
Hatua hii ilionekana kama kumkata miguu Bw Sifuna ambaye amekuwa akishiriki mahojiano na vituo mbalimbali kulemea utawala wa Rais Ruto.