Habari za Kitaifa

Ruto sasa amtegemea Kiunjuri kumrejeshea kura za Mlima Kenya

Na GITONGA MARETE, MWANGI NDIRANGU August 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri amegeuka mhimili wa Rais William Ruto katika jitihada zake za kuhakikisha kuwa anarejesha uungwaji mkono aliokuwa nao Mlima Kenya katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Bw Kiunjuri ni kati ya wanasiasa wazoefu wenye tajriba kuu akihudumu muhula wake wa nne bungeni mbali na kwamba alihudumu kama waziri wa Kilimo katika utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Rais Ruto anamtegemea sana Bw Kiunjuri ili kuupata uungwaji mkono wa Mlima Kenya Magharibi huku Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki akiwekewa matumaini ya kumvutia Mlima Kenya Mashariki.

Baada ya kujiunga na siasa akiwa na umri mdogo, Bw Kiunjuri amefanya kazi na marais watatu na alikuwa kati ya wanasiasa walioaminiwa sana na Rais Mwai Kibaki (sasa marehemu).

Wakati wa kampeni za kuunga mkono kurasmishwa kwa katiba mpya ya mwaka wa 2010, Bw Kiunjuri alikuwa kati ya wanasiasa ambao Bw Kibaki aliwapa jukumu la kuhakikisha Mlima Kenya unapitisha rasimu hiyo ya katiba.

Bw Kiunjuri ana kipaji cha ulumbi na hutema sana misemo kwa lugha ya Agikuyu, mikutano yake mingi ikionekana kusisimua hadhira yake.

Mnamo 2022 akisimama na chama chake cha TSP, alihimili mawimbi makali ya UDA Mlima Kenya akimbwaga aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Amin Deddy wa UDA.

Kutoka 2013-2022 hakuwa mbunge baada ya kushindwa katika ugavana mnamo 2013, lakini 2017 hakusimama. Kisha aliteuliwa waziri wa Kilimo.

Tangu kurejea bungeni 2022, Bw Kiunjuri ni kati ya wanasiasa ambao wamekuwa na uhasama mkubwa na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.

Mwezi uliopita, Bw Gachagua akiwa Amerika alimshutumu Bw Kiunjuri akisema serikali inamtumia pamoja na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah kuendeleza dhuluma dhidi ya vijana wa Mlima Kenya.

Hivi majuzi mbunge huyo aliteuliwa mwenyekiti wa kundi la wabunge ambao ni waaminifu kwa serikali ya Kenya Kwanza.

Sasa kibarua cha kwanza kwa Bw Kiunjuri ni kuhakikisha Kenya Kwanza inatwaa kiti cha eneobunge la Mbeere Kaskazini ambacho kilisalia wazi baada ya Geoffrey Ruku kuteuliwa waziri na Rais Ruto.

Matokeo ya uchaguzi huo yatatumika kuonyesha iwapo Rais Ruto bado ana umaarufu Mlima Kenya.

Wakati wa kuondolewa kwa Bw Gachagua serikalini mnamo Oktoba mwaka jana, Bw Kiunjuri aliunga mkono hoja ya kumtimua katika unaibu rais na hata akawarai wabunge wengine kutoka Kaunti ya Laikipia waunge mkono hoja hiyo.

Licha ya wabunge waliounga mkono Bw Gachagua kupata ugumu wa kuhutubu kwenye hafla za umma na kuzomewa, Bw Kiunjuri amekuwa mkakamavu akitumia majukwaa na mikutano kusema hawezi kufuata mkondo wa kisiasa wa aliyekuwa naibu huyo wa rais.

“Sisi hatutatumia siasa za kibabe bali tutatumia siasa za kuwafikishia watu wetu miradi ya maendeleo,” akasema Bw Kiunjuri katika misururu ya mikutano ambayo amekuwa akiendeleza eneobunge lake.