Asencio hatarini kutupwa gerezani miezi 30, kisa kanda za ngono!
MWENDESHA mashtaka wa umma anataka beki wa Real Madrid, Raul Asencio, afungwe jela miaka miwili na nusu iwapo atapatikana na hatia ya kusambaza kanda ya ngono iliyohusisha mtoto mdogo.
Mnamo Februari mwaka huu ilifichuliwa kuwa Asencio, 22, angeshtakiwa mahakamani katika visiwa vya Canary baada ya kudaiwa kusambaza picha na video za uchi wa mtoto mdogo na msichana mwingine.
Kwa mujibu wa Jarida la The Athletic, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Uhispania imedai wachezaji wawili wa zamani wa akademia ya Real walishiriki mapenzi kwa maelewano na wasichana hao wawili, akiwemo mtoto mdogo.
Wanadaiwa kupiga picha za tukio hilo bila ridhaa ya mtoto huyo na msichana mwingine aliyehusika. Kisha Asencio anadaiwa kuomba kutumiwa video za anasa yao kabla kuzionyesha mtu mwingine.
Hii inamaanisha kwamba alikiuka mara mbili Kifungu 77 cha Kanuni ya Jinai ya Uhispania inayohusiana na faragha, ikiwa atapatikana na hatia.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uhispania ni miongoni mwa makinda wanne wa akademia ya Real waliohusika katika kisa hicho kinachoendelea kuchunguzwa, lakini ndiye pekee angali klabuni humo.
Wasichana hao wawili husika wanadaiwa kupatwa na msongo wa mawazo baada ya tukio hilo. Wanasemekana kumtaka Asencio kulipa kila mmoja wao fidia ya Sh757,000.
Mapema mwaka huu, Asencio alitoa taarifa akikanusha vikali kufanya makosa yoyote.
“Sijawahi kushiriki tukio lolote linalokiuka uhuru wa kijinsia wa mwanamke yeyote, achia mbali watoto wadogo wa kike,” alisema.