Habari za Kitaifa

Uhuru: Nitaunga mkono Raila kuwania urais ikiwa ataachana na Ruto

Na MOSES NYAMORI August 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha Jubilee kimetangaza kuwa kiko tayari kumuunga mkono Kinara wa ODM Raila Odinga kuwania urais 2027 kikisema kuwa bado kinamtambua kama Kiongozi wa Muungano wa Azimio.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, amesema kuwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, jana aliwaambia kuwa yupo tayari kumuunga Raila mnamo 2027 mradi tu asambaratishe uhusiano wake na utawala wa sasa.

Bw Kenyatta jana aliongoza mkutano wa Kamati Kuu ya Jubilee kwenye makao makuu ya chama hicho, kikao kilichofanyika baada ya mrengo wake kushinda kesi ya mzozo wa uongozi wa Jubilee mahakamani.

“Bado tunamtambua Raila kama kiongozi wa Azimio. Na kama muungano tunaamua mwelekeo wetu, hata hivyo nakuambia tuko na Tinga (Raila) hadi hali iwe vingine. Raila ndiye kiongozi wetu na Uhuru mwenyekiti wetu,” akasema Bw Murathe.

“Watu pia wanaweza kuamua tuunde muungano mpya na tuwashirikishe viongozi wengine zaidi,” akaongeza.

Chama cha Jubilee kinaonekana kimeshaajishwa na mizozo inayotokota ndani ya ODM kuhusu uungwaji mkono wa Serikali Jumuishi ndiposa bado kinashabikia Raila.

Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna amekuwa akishutumu hatua ya chama kushirikiana na Rais William Ruto huku kundi la wabunge waaminifu kwa Bw Odinga nalo likisema lazima washirikiane na utawala huu hadi 2027.

Akimsifia Bw Odinga, Bw Murathe alisema hatua yake ya kuficha kadi kuhusu mwelekeo wa kisiasa atakaouchukua unawawekea imani kuwa bado wanaweza kufanya kazi na ye.

“Hata ukimwaangalia jinsi anavyozungumza na mwonekano wake, utaona tu hataunga serikali hii. Hakuna vile Sifuna angekuwa akizungumza jinsi anavyofanya bila baraka za Raila,” alisema.

Aliongeza, “Nimeambiwa kuwa naibu viongozi wa ODM pia wako na Sifuna. Raila ni gwiji wa mchezo huu na anajua kuteka hisia za watu kabla ya kutoa mwelekeo wake wa kisiasa.”

Kuhusu madai kuwa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i analenga kutumia chama hicho kuwania urais, Bw Murathe alisema hakuna jambo kama hilo limejadiliwa na kuafikiwa na chama.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Jeremiah Kioni, amenukuliwa mara si moja akisema kuwa Dkt Matiangí ndiye atapeperusha bendera ya chama hicho.

Japo Jubilee bado ina imani kuwa Raila atajibwaga debeni, kiongozi huyo wa ODM hajatangaza azma yake na amesema ataendelea kushirikiana na serikali ya sasa hadi 2027.

Raila amesimama urais mara tano na mwenyewe amekuwa akisema ushirikiano wake na UDA ni kuhakikisha kuwa serikali inasalia dhabiti.

“Hatujasema tutaendelea kufanya kazi na UDA baada ya 2027. Haya ni mambo ambayo tutayajadili wakati ukifika na wanachama ndio wataamua,” akasema Bw Odinga kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Wiki jana, Bw Kenyatta alionekana kuchangamkia sana Rais Ruto kwenye ikulu ya Nairobi, tukio ambalo lilifasiriwa na baadhi ya Wakenya kuwa wawili hao nao wanapanga kuzika tofauti zao na kuridhiana kisiasa.