Habari za Kitaifa

Ripoti yafichua mabilioni yanavyopotea kupitia e- Citizen

Na  DAVID MWERE August 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu, amefichua dosari kubwa katika usimamizi wa jukwaa la malipo la kidijitali la serikali – e-Citizen – hali inayoweza kuwa imesababisha kupotea kwa zaidi ya Sh10 bilioni zilizolipwa na Wakenya ili kupata huduma za umma.

Katika  ripoti ya ukaguzi maalum iliyowasilishwa mbele ya Bunge la Taifa, Mkaguzi Mkuu alionya kuwa jukwaa hilo kuthibitiwa  na muuzaji wake ni hatari  na tishio la kimkakati kwa utoaji wa huduma kwa umma.

Udhaifu huo unaongeza uwezekano wa mifumo kuharibika, uvujaji wa data, na kukiukwa kwa masharti ya usalama wa taarifa, huku mashirika husika ya serikali yakishindwa kuchukua hatua.

Naibu Mkaguzi Mkuu, Bw Isaac Ng’ang’a, alipowasilisha ripoti hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma (PAC), alisema ukaguzi huo haukuonyesha tu kupotea kwa mabilioni ya pesa za walipa ushuru, bali pia ulifichua kuwa Wakenya walitozwa ada za juu kupita kiasi – wakilipa Sh2.6 bilioni  zaidi walipotumia jukwaa hilo kupata huduma.

Kutokana na matokeo hayo, PAC imewaita makatibu wa wizara muhimu watoe maelezo kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma. Miongoni mwao ni Dkt Chris Kiptoo (    Wizara ya Fedha), Dkt Belio Kipsang (Uhamiaji na Huduma za Raia), na Bw John Tanui (ICT).

“Kile ambacho Mkaguzi Mkuu ametufichulia leo ni janga,” alisema Mbunge wa Aldai, Bi Marianne Kitany. Naye Mbunge wa Rarieda, Otiende Amolo, alitaja hali hiyo kuwa ni “utapeli wa hali ya juu.”

Ukaguzi maalum huo ulihusisha miaka ya fedha ya 2021/22, 2022/23, na 2023/24, ambapo ulifichua mapungufu makubwa katika mfumo huo, ikiwemo malipo yasiyoeleweka ya ukarabati, risiti ambazo hazikuonyeshwa, mapato kuelekezwa bila idhini, na kutolewa haramu kwa pesa kutoka kwa nambari ya malipo ya M-Pesa 222222.

Hapo awali, jukwaa la e-Citizen lilikuwa mradi wa serikali uliogharimiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) la Benki ya Dunia, ambalo lilikabidhi Webmasters Kenya Ltd jukumu la kuunda na kulitunza.

Mnamo 2017, IFC ilikabidhi mali zote ikiwemo mikataba na msimbo wa chanzo kwa Wizara ya Fedha

Hata hivyo, iligundulika kwamba Januari 13 2023, Wizara ya ICT iliingia tena katika makubaliano na Webmasters, jambo lililoashiria kuwa udhibiti wa jukwaa hilo ulikuwa umerejea kwa muuzaji  bila maelezo yoyote.

“Haikufafanuliwa ni jinsi gani umiliki na udhibiti wa jukwaa la e-Citizen ulirejea mikononi mwa muuzaji baada ya  tayari kukabidhiwa Wizara ya Fedha na IFC mwaka 2017,” inasema ripoti ya ukaguzi huo.

Tafsiri: BENSON MATHEKA