Tanzania imefunga mabao mawili tu CHAN, yaishinda Mauritania kibahati
TANZANIA Jumatano jioni ilinusurika kwenye mchezo wake wa pili, ikiifunga Mauritania 1-0 katika kipute cha Kombe la Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024).
Shomari Kapombe alifunga bao hilo dakika ya 89, baada ya mabeki wa Mauritania kushindwa kuondoa mpira ndani ya kijisanduku. Mchuano huo ulipigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ambao ulifura mashabiki wengi wa Taifa Stars.
Tanzania ilishinda mechi ya kwanza Jumamosi iliyopita ikiipiga Burkina Faso 1-0 katika uwanja huo huo.
Taifa Stars sasa inaongoza Kundi B kwa alama sita huku Burkina Faso iliyokuwa imefunga Jamuhuri ya Afrika ya Kati 4-2 kwenye mechi nyingine ya Kundi B Jumatano, ikiwa ina alama tatu.
Madagascar na Mauritania ambazo pia zipo kundi hilo zina alama moja kila moja huku Jamuhuri ya Afrika ya Kati ikiwa haijaambulia alama zozote.
Katika mechi dhidi ya Mauritania, Tanzania haikuonyesha makali sana na walitumia tu kuchanganyikiwa kwa mabeki wa wapinzani wao kufunga bao hilo kipindi cha pili kikibakia sekunde 60 kukamilika.
Idd Nado alipiga pasi ambayo haikuzuiwa na mabeki wa Mauritania ndipo ikaangukia Shomari Kapombe aliyeachilia fataki iliyomlemea Abderrahmane Sarr kunyaka. Kwenye dakika zilizoongezwa, Tanzania ilionekana kumakinikia kulinda bao hilo huku uwanja ukilipuka baada ya kipenga cha mwisho.
Taifa Stars sasa ipo pazuri kufuzu robo fainali kwa kuwa itakuwa ikizipiga dhidi ya Madagascar na Jamuhuri ya Afrika ya Kati ambazo zinaonekana kama wapinzani dhaifu, kukamilisha mechi ya makundi.