Hali yadorora Haiti licha kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya
HALI ya usalama nchini Haiti imezidi kuwa mbaya kwa miezi minne iliyopita, ikisababisha vifo vya watu 1,520, jambo ambalo linaonyesha changamoto kubwa inayokabili kikosi cha usalama cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya.
Hali hii inajiri wakati Amerika imesitisha shughuli za ubalozi wake jijini Port-au-Prince kutokana na mapigano katika eneo la Tabarre.
Amerika pia imetoa onyo kwa raia wake kuepuka kusafiri kuenda Haiti.
Ingawa mwezi Juni ulikuwa mwaka mmoja tangu askari polisi wa Kenya walipoanza kuhudumu nchini humo, hali imezidi kuwa mbaya na ghasia, unyanyasaji wa kingono, na kuwahamisha watu kwa nguvu umeongezeka.
“Mashambulio ya magenge katika mikoa ya Artibonite, Centre na mji mkuu yanaendelea kusababisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kusababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu,” alisema Ulrika Richardson, wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Haiti (BINUH)
Tangu Januari hadi Julai, watu zaidi ya milioni 1.3 wamehama makazi, wengi wakiwa wanawake na watoto.
Maafisa wa kikosi cha usalama cha kimataifs, wakiwemo maafisa wa Kenya, wameshindwa kufanikiwa kutokana na ukosefu wa vifaa.
Asilimia 64 ya waathirika waliuawa wakati wa operesheni za usalama, na zaidi ya theluthi moja ya vifo hivyo vilihusisha mashambulizi ya kutumia droni zenye mabomu.
Umoja wa Mataifa umelaani operesheni hizi kwa kusababisha vifo vya raia, ambapo asilimia 15 ya vifo vimetokana na operesheni zisizofanikiwa vya kikosi cha usalama.
Kenya imempoteza afisa mmoja, Samuel Tompoi Kaetuai, aliyepigwa risasi na kuuawa Februari 2025. Afisa mwingine, Benedict Kuria, bado hajapatikana.
Hata hivyo, kikosi kinaendelea licha ya hali kuwa mbaya zaidi.
Mapigano ya hivi karibuni karibu na Ubalozi wa Amerika yanahusishwa na hasira za kukamatwa kwa seneta wa zamani wa Haiti, Nenel Cassy, anayekabiliwa na mashtaka ya kusaidia magenge, kufadhili makundi haramu, kufanya njama dhidi ya usalama wa taifa na mauaji.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA