Ruto, Raila waweka mikakati ya kulinda ukuruba kuzuia nyufa kutokea
RAIS William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wametoa ishara za wazi kwamba chama tawala cha UDA na ODM vinafuma muungano wa kisiasa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Viongozi hao wawili wametangaza mpango wa kufanyika kwa mikutano ya pamoja ya Kundi la Bunge la Kenya Kwanza na ODM kila robo mwaka ili kutathmini utekelezaji wa mkataba wa vipengele 10 kati ya vyama vyao.
Haya yanajiri huku Rais akifanya lolote kuzima upinzani dhidi ya makubaliano ya kisiasa kati ya UDA na ODM, kama mkakati wa kushawishi chama hicho cha Chungwa ambacho bado kina uungwaji mkono mkubwa katika maeneo ya Nyanza, Magharibi na Pwani.
Vyanzo vya ndani vinasema kuwa Rais analenga kushughulikia malalamishi yaliyoibuliwa na baadhi ya maafisa wa juu wa ODM, yakiwemo madai ya fidia kwa waathiriwa wa maandamano, ugavi zaidi wa rasilimali kwa kaunti, pamoja na kukomesha mauaji na utekaji nyara unaohusishwa na polisi kama njia ya kudhibiti uasi dhidi ya makubaliano yake ya kisiasa na Bw Odinga.
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna ambaye, yaonekana anaungwa mkono na Bw Odinga, amekuwa mstari wa mbele kushinikiza ODM ijiondoe kwenye makubaliano hayo kwa sababu UDA imeshindwa kutekeleza yaliyokubaliwa.
ODM chini ya Bw Odinga imeeleza kuwa utekelezaji kamili wa Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa vipengele 10 ndio utakaoamua uwezekano wa muungano wa kabla ya uchaguzi wa 2027 kubuniwa.
Chama pia kinaamini kuwa kumvumisha Rais Ruto kunawezekana tu ikiwa makubaliano hayo yatatekelezwa.
Rais Ruto na Bw Odinga mnamo Jumatano waliunda kamati ya kiufundi ya wanachama watano kusimamia utekelezaji wa vipengele 10 pamoja na mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO).
NADCO ilikuwa majadiliano ya pande mbili kati ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja-One Kenya kufuatia maandamano yaliyoongozwa na upinzani mwaka wa 2023.
Kamati hiyo ya kiufundi itaongozwa na aliyekuwa seneta mteule wa ODM Agnes Zani na inajumuisha Fatuma Ibrahim, Kevin Kiarie, Gabriel Oguda, na Javas Bigambo kama wanachama.
Ripoti ya NADCO ilipendekeza mageuzi makubwa, ikiwemo kuanzishwa kwa Ofisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mapendekezo mengi ya ripoti hiyo isipokuwa ya kubadilisha na kuunda upya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), bado hayajatekelezwa.
Mbali na kuahidi kuhakikisha utekelezaji kamili wa ripoti ya NADCO, Rais pia ameahidi kulinda haki ya maandamano ya amani na kulipa fidia kwa waathiriwa wa maandamano pamoja na kupambana na ufisadi.
Ajenda nyingine zitakazoharakishwa ni ushirikishaji katika huduma za umma, kulinda na kuimarisha ugatuzi pamoja na kukuza maisha ya vijana.
Dkt Ruto na Bw Odinga, “kama viongozi wa vyama walikubaliana kuanzisha mfumo mpana wa ushirikiano kati ya miungano yote ya kisiasa na wadau wengine muhimu,” inasema sehemu ya taarifa ya pamoja waliyoisaini wawili hao.
“Katika kutekeleza majukumu yake chini ya mwongozo wa viongozi wakuu (Ruto na Raila), kamati itafanya mashauriano ya kina na ya kujumuisha umma na wadau wote muhimu, ikiwemo mihimili ya serikali, idara za serikali, tume huru, mashirika ya kiraia, taasisi za kidini na sekta binafsi.”
Viongozi hao wawili wanataka kuhakikisha kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo unaongozwa na mitazamo mbalimbali ili kushughulikia mahitaji na matarajio ya Wakenya.
Kamati hiyo imepewa maagizo ya kuanza kazi mara moja na itakuwa inawasilisha ripoti kwa viongozi hao kila baada ya miezi miwili.
Pia itawasilisha ripoti ya maendeleo kwa Kundi la Pamoja la Wabunge wa Kenya Kwanza na ODM kila robo mwaka.
“Kundi la Wabunge litafanya kikao chake cha kwanza mnamo Agosti 18, 2025. Ripoti ya mwisho na ya kina kuhusu hali ya utekelezaji wa makubaliano itatolewa kwa umma mnamo Machi 7, 2026, ikiwa ni kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutiwa saini kwa makubaliano hayo,” walisema viongozi hao wawili.
Bw Odinga tayari amekanusha uwezekano wa kujiondoa mapema katika serikali jumuishi iliyoanzishwa mwaka jana, ambayo baadhi ya washirika wake wa karibu waliteuliwa kwenye baraza la mawaziri na na wengine kama washauri. Alisisitiza kuwa anaunga mkono kikamilifu Rais Ruto, angalau hadi uchaguzi mkuu ujao.
“Tumesema kuwa tupo ndani ya serikali hadi 2027. Baada ya 2027 ni mambo ambayo tutajadili kwa wakati ufaao, na uamuzi utafanywa na wanachama wa chama, si Raila Odinga peke yake,” alisema Bw Odinga katika mahojiano na Taifa Leo.
Bw Odinga pia amepuuza uvumi unaoendelea kuhusu uwezekano wa Rais Ruto kuchaguliwa kwa awamu ya pili, akisisitiza kuwa ni wananchi pekee wanaoweza kuamua kupitia kura.
“Si suala la muhula mmoja au miwili. Swali la kweli ni: nani anaamua? Ni wananchi wenye mamlaka kupitia kura,” alisema.
Alisisitiza kuwa matokeo ya uchaguzi yanategemea utendakazi, si kauli mbiu za kisiasa au vitisho, huku akieleza kujitolea kwake katika utekelezaji wa makubaliano ya UDA-ODM.
“Unaweza kupata muhula mmoja, miwili, au hata nusu ya muhula. Hatimaye, ni wananchi watakaoamua kupitia uchaguzi.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti na Ugavi Sam Atandi alidokeza uwezekano wa tangazo la “Ruto-Tosha” kutokana na muungano wa kisiasa kati ya ODM na UDA kumsaidia Rais kupata muhula wa pili.
Mbunge wa Alego Usonga, aliyekuwa mgeni katika hafla ya kuwawezesha wanawake huko Gem, Yala, alisema vyama hivyo viwili vitashirikiana na kumuunga mkono Rais Ruto katika azma yake ya muhula wa pili.
“Tuna deni kwa Rais Ruto la shukrani, alisimama na Raila Odinga mwaka 2007 katika uchaguzi. Raila akawa Waziri Mkuu.”
Mbunge wa Uriri Mark Nyamita alisema: “Hatujawahi kuona rais ambaye ametujali kama Ruto. Hakuna atakayetufanya tubadilishe nia.”
TAFSIRI: BENSON MATHEKA