Dimba

DR Congo yalemea Zambia na kupata ushindi wa kwanza CHAN 2024

Na CECIL ODONGO August 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JAMUHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Alhamisi iliweka nyuma masaibu ya kupigwa na Kenya na ikaishia kushinda Zambia 2-0 kwenye mechi yake ya pili ya kuwania ubingwa wa Kombe la Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za nyumbani (CHAN).

DR Congo ilikuwa imechapwa 1-0 na Kenya mnamo Jumapili katika uwanja wa MISC Kasarani katika mechi ya kwanza ya Kundi A.

Austin Odhiambo alifunga bao hilo kipindi cha kwanza. Hata hivyo, DR Congo ambao ni mabingwa wa 2009 na 2016 walionyesha kuwa wao si rahisi kwenye kundi hilo, wakifunga mabao mawili na kujizolea alama zao tatu za kwanza.

The Leopards walichukua uongozi dakika ya 51 baada ya Ibrahim Batobo kupata nafasi na kuachilia fataki kali iliyomlemea kipa wa Zambia Willard Mwanza kunyaka.

Bao hilo liliwaamsha mashabiki wengi wa DRC ambao walikuwa wamefurika Nyayo kushangilia timu yao ikizingatiwa wengi wa raia wa taifa hilo wanaishi hapa nchini.

Bana ba Congo walipata bao la pili dakika ya 71 kupitia Malanga Harso Mwaku na wakaishia kulinda uongozi wao hadi kipenga cha mwisho.

DR Congo, Morocco zina alama tatu pamoja na Kenya ambayo ilitarajiwa ingechuana na Angola baadaye jana kwenye mechi nyingine ya Kundi A.