Zogo lanukia serikali kuu ikipanga kupokonya kaunti jukumu la kukusanya mapato
KUANZIA mwaka ujao, serikali za kaunti hazitaruhusiwa tena kukusanya mapato yao kufuatia mipango ya serikali kuu ya kuanzisha mfumo mmoja kama jukwaa la kitaifa la kushughulikia ukusanyaji wa mapato yote ya kaunti, kwa lengo la kuimarisha uwazi na ufanisi katika sekta hiyo.
Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi, aliambia Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Umma (PAC) kwamba maandalizi ya kuanzisha mfumo huo yako katika hatua za mwisho na utekelezaji wake utaanza Desemba mwaka huu.
“Tutakuwa na taasisi moja tu ya ukusanyaji mapato, sawa na jinsi serikali kuu inavyofanya. Kuna mazungumzo yanayoendelea kupitia Baraza la Bajeti na Uchumi baina ya Serikali Kuu na Kaunti (IBEC) kabla ya utekelezaji rasmi,” alisema Bw Mbadi mbele ya kamati inayoongozwa na Seneta Moses Kajwang’.
Alifafanua kuwa mfumo mpya utasaidia kukomesha visa ambapo baadhi ya kaunti hukusanya mapato na kuyatumia papo hapo bila kuweka kumbukumbu, huku nyingine zikidanganya kuhusu kiasi halisi kilichokusanywa.
“Tumelijadili suala hili kupitia IBEC, ingawa limepingwa na Baraza la Magavana. Hata hivyo, tumeanza kuona matumaini. Hatuwezi kuwa na mifumo 48 tofauti ya ukusanyaji mapato,” Bw Mbadi alisisitiza.
Waziri huyo alitetea hatua hiyo akisema kuwa haikiuki uhuru wa kaunti, kwani Katiba inatambua mamlaka ya Wizara ya Fedha kuunda mifumo ya kifedha nchini.
“Ingawa kaunti zina uhuru fulani, Katiba inaruhusu Wizara ya Fedha kuanzisha mifumo ya kifedha nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa kabla ya kuanza kwa mfumo huo mpya, kaunti zote 47 zitahusishwa kikamilifu kwani ndizo zitakazokuwa watumiaji wa mwisho wa mfumo huo.
“Hatutawapa tu mfumo bila ushauriano. Tunahitaji kuwahusisha ili wasije wakaukataa kimakusudi,” alisema.
Kwa maandalizi ya utekelezaji, Wizara ya Fedha tayari imeandikia kaunti kutaka taarifa kuhusu mifumo yao ya sasa ya ukusanyaji mapato, majina ya wasambazaji wa mifumo hiyo, na muda wa kumalizika kwa kandarasi zao.
Mbadi pia aliambia kamati hiyo ijiandae kwa mageuzi makubwa katika ukusanyaji wa mapato, ambayo yatawasilishwa bungeni.
“Kuna mapengo mengi tunayopaswa kuziba. Tunapanga kuanzisha mageuzi mengi muhimu,” alisema.
Alisema ushuru unaokusanywa kutoka kwa wananchi unapaswa kuanza kuwanufaisha moja kwa moja.
“Wakenya wanalalamika kuwa wanatozwa ushuru bila kuona huduma. Hii ni kwa sababu pesa nyingi zinapotea katika mianya ambayo tunapaswa kuifunga,” alisema.
Maseneta waliunga mkono mpango huo wakisema kuna baadhi ya watu wanaowania nyadhifa za ugavana kujitajirisha binafsi badala ya kuhudumia wananchi.
“Tusiruhusu kaunti kuwa sehemu ya kujitajirisha. Tuko tayari kushirikiana kuhakikisha mfumo huu wa ukusanyaji mapato unafanikishwa,” alisema Seneta Kajwang’.
Seneta wa Isiolo, Fatuma Dullo, alisema hali ya sasa ya ukusanyaji mapato katika kaunti ni ya kusikitisha.
Iwapo mfumo huo mpya utaidhinishwa, utaziba mianya ambayo magavana wamekuwa wakitumia kufungua akaunti nyingi ambazo hazikaguliwi ambapo mapato yanapotelea.
Ripoti ya Msimamizi wa Bajeti kwa robo ya kwanza ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 (Julai–Oktoba) ilifichua kuwa kaunti zinaendesha jumla ya akaunti 2,421 za benki kinyume na sheria.
Kaunti zenye idadi kubwa zaidi ya akaunti ni pamoja na Bungoma (321), Baringo (292), Migori (208), na Kwale (165).
Sheria za fedha za umma inazitaka kaunti kufungua na kuendesha akaunti zao kupitia Benki Kuu ya Kenya (CBK), lakini nyingi zimekiuka agizo hilo, hatua inayotishia uwazi na uwajibikaji.
TAFSIRI: BENSON MATHEKA