Heri mzoee ndoa yetu hii, Ruto na Raila waambia wapinzani
Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga wameahidi kuendelea kushirikiana ili kuimarisha maendeleo na uthabiti wa taifa.
Viongozi hao wawili walisema wazi kuwa hawatengani hivi karibuni, angalau hadi uchaguzi mkuu wa 2027, wakisisitiza kuwa ushirikiano wao unalenga kuleta utulivu na ustawi wa kiuchumi kwa wananchi.
Rais Ruto na Bw Odinga walianza rasmi kushirikiana Machi 2025 waliposaini makubaliano (MOU) kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kitaifa,na kushughulikia changamoto za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Akizungumza katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Karachuonyo, Bi Phoebe Asiyo, katika Kijiji cha Wikondiek, Kaunti ya Homa Bay mnamo Ijumaa, Rais Ruto alimtaja Bw Odinga kuwa mzalendo na kiongozi aliyejitolea kuendeleza taifa.
“Mwenzangu Raila amesema yote kwa njia nzuri. Ana nafasi muhimu katika historia, maendeleo na mustakabali wa taifa letu. Mimi naamini Kenya ni nchi kuu, na hilo litategemea juhudi zenu wananchi,” alisema Rais Ruto.
Aliongeza kuwa Kenya ina uwezo mkubwa wa kustawi zaidi ikiwa itaelekeza nguvu katika umoja, kukabiliana na ukosefu wa ajira na mageuzi ya kilimo ili kuondoa njaa.
“Tuna nafasi ya kihistoria kuinua taifa letu. Tumejipanga vizuri, na kwa sababu hiyo tulisaini ajenda ya vipengele kumi,”alisema.
Rais alieleza kuwa serikali yake imeanza kutekeleza makubaliano ya MOU na tayari ameunda timu kutathmini fidia kwa waathiriwa wa maandamano ya awali. Pia ameunda kamati ya kutekeleza mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Majadiliano ya Kitaifa (NADCO).
‘Tumeanza safari. Tumelipa fedha zote za kaunti kutoka mwaka uliopita, na Jumatatu fedha za Julai zitatumwa kwa kaunti,” alisema Ruto.
Aliagiza wabunge wa Kenya Kwanza kushirikiana na wenzao wa ODM kuandaa miswada na bajeti zitakazowezesha utekelezaji wa makubaliano hayo. Kikao cha pamoja cha wabunge wa UDA na ODM kinatarajiwa wiki ijayo.
‘Hatuchezi kamari. Tunajua tulipotoka na tunakoelekea. Lazima tulinde amani na uthabiti wa taifa letu,” aliongeza Rais.
Bw Odinga naye alisisitiza kuwa kushirikiana na Kenya Kwanza ni hatua ya lazima ili kuzuia taifa kutumbukia katika migogoro kama inavyoonekana katika baadhi ya mataifa ya Afrika na Mashariki ya Kati.
“Watu wasioelewa historia huongea ovyo. Tumeona yaliyotokea katika mataifa ya Kiarabu. Hatuwezi kuruhusu hayo kutokea hapa,” alisema Bw Odinga.
Alisisitiza kuwa uamuzi wa kushirikiana na Rais Ruto ulikuwa wa lazima kutokana na hali ya kisiasa wakati huo.
“Lazima tuboreshe muundo wa serikali ili kuhakikisha wananchi wanaishi vyema – chakula, makazi, elimu na huduma za afya kwa wote,” alisema.
Licha ya kuunga mkono serikali, Bw Odinga alitaja masharti kadhaa, ikiwemo kupunguzwa kwa gharama ya maisha. Pia alikemea matumizi ya nguvu kupita kiasi na polisi dhidi ya raia.
“Polisi hawapaswi kuua. Wakamate washukiwa na kuwapeleka kortini, si kuwaua,” alisema, akisisitiza kuwa utekelezaji wa MOU lazima ufuatwe kikamilifu.
MOU hiyo pia ilipendekeza fidia kwa waathiriwa wa maandamano, hasa wale walioumia au kupoteza jamaa zao tangu mwaka wa 2017. Bw Odinga alisema utekelezaji wa fidia hiyo utafuatiliwa kupitia kamati ya pamoja
Aliwatahadharisha wakosoaji wa ushirikiano wake na Ruto kuacha kuingilia mchakato huo, huku akimkemea Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Lakini pia alifafanua kuwa ODM na UDA watakuwa na fursa ya kujieleza mbele ya wananchi kuelekea uchaguzi wa 2027.
“Nina hakika, wakati ukifika, kila mmoja wetu ataeleza mpango wake kwa Wakenya. Wataamua ni nani wa kufuata,” alisema Bw Odinga.