Habari za Kitaifa

Wiki ya nuksi ajali zikiua 50 nchini

Na  WAANDISHI WETU August 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kenya inashuhudia mwezi mwingine wa Agosti wenye majonzi baada ya msururu wa ajali mbaya kusababisha vifo vya watu wasiopungua 50 kwa wiki moja kufikia Agosti 9, 2025.

Ajali hizi zimekuwa zikifuatana kwa kasi ya kushtua, zikitokea barabarani, kwenye reli na hata angani hali inayofufua kumbukumbu chungu za Agosti zilizopita ambazo zimekuwa zikihusishwa na huzuni ya kitaifa.

Ajali ya hivi punde ilitokea jana alfajiri, Agosti 9, katika eneo la Korompoi barabara kuu ya Kitengela–Isinya. Matatu ya Nailepu Sacco iligongana ana kwa ana na lori, na kuua watu saba papo hapo wanaume watatu na wanawake wanne. Wengine kadhaa walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini. Mtu wa nane alifariki akipokea matibabu hospitalini.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Isinya, Simon Lokitari, alithibitisha vifo hivyo na kutoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuwa waangalifu ili kuepuka ajali.

Amesema visa vya madereva kuendesha magari kwa kasi ni vingi kwa sababu wanadhani kuwa barabara hiyo haina msongamano mkubwa wa magari.

“Ni asubuhi ya huzuni sana. Tumepoteza watu saba wanawake wanne na wanaume watatu, wote wamefariki papo hapo. Kuna waliojeruhiwa vibaya na wamekimbizwa katika hospitali mbalimbali kwa matibabu,” alisema Bw Lokitari.

Ajali hii ya Kitengela ilifuatia ya kuhuzunisha zaidi Agosti 8, ambapo basi iliyobeba waombolezaji kutoka mazishini ilianguka kwenye barabara ya Kisumu–Kakamega, na kuua watu 25.

Mnamo Agosti 7, ndege ya shirika la matibabu la AMREF ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi. Watu wanne waliokuwa ndani ya ndege hiyo waliaga dunia pamoja na watu wawili waliokuwa ndani ya jengo ilikoanguka.

Maafisa wa polisi wanasema kuwa uchunguzi wa pamoja na mamlaka ya usafiri wa anga (KCAA) umeanzishwa mara moja.Siku hiyo hiyo, basi la wafanyakazi wa Kenya Pipeline liligongana na gari moshi karibu na Naivasha na kuua watu wanane.

Mnamo Agosti 6, mwanasiasa wa zamani wa Kisii, Askofu Josiah Onyancha, na mkewe waliaga dunia kwenye ajali huko Narok walipokuwa wakielekea kwenye mahafali ya mwana wao.

Kufuatia ajali hizi Rais William Ruto amewaagiza maafisa wanaohusika na uchukuzi kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama wa abiria na watumiaji barabara.Katika taarifa baada ya ajali iliyoangamiza watu 25 kaunti ya Kisumu, Rais Ruto aliagiza mashirika husika kuchunguza kwa kina kilichoisababisha.

“Sala zetu ziko pamoja na waathirika wa ajali mbaya iliyotokea usiku wa kuamkia jana kwenye barabara ya Kisumu-Kakamega,” alisema Rais Ruto.

“Tunahimiza maafisa usalama barabarani wachukue hatua za haraka kuwawajibisha wote wanaohusika na uzembe wowote uliosababisha ajali hii na kushughulikia ukiukaji wote wa sheria za usafiri ili kuhakikisha usalama barabarani nchini kote.”

Waziri wa Barabara, Davis Chirchir, pia alitangaza kuwa tathmini kamili ya usalama itafanyika ili kuandaa mikakati madhubuti ya kuzuia ajali kama hizi kutokea tena.