Taharuki polisi wakivamia na kuzingira nyumba ya Mbunge Jayne Kihara Naivasha
Taharuki ilitanda mjini Naivasha Jumamosi asubuhi baada ya maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami kuzingira nyumba ya Mbunge wa Naivasha, Bi Jayne Kihara, katika eneo la Maraigushu, katika kile kinachoonekana kama msako wa wafuasi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachohusishwa na Rigathi Gachagua.
Bi Kihara alisema kuwa polisi walifunga barabara zinazoelekea nyumbani kwake na kufunga lango kuu, kuzuia wageni wake kuingia.
“Badala ya serikali kuwatuma polisi kukabiliana na walanguzi wa watoto huko Maai Mahiu, imeamua kunilenga mimi mwanamke mmoja asiye na hatia,” alisema kwa hasira.
Kamanda wa Polisi wa Naivasha, Bw Anthony Keter, alidai kuwa Bi Kihara hakuwa ametoa taarifa kwa polisi kuhusu kikao hicho, lakini mbunge huyo alipinga vikali madai hayo.
“Je, kukutana na wapiga kura wangu katika nyumba yangu binafsi kunahesabiwa kuwa mkutano haramu?” alihoji Bi Kihara.
Mbunge huyo alikabiliana na afisa mmoja wa polisi, akitaka kujua kwa nini walizuia wageni wake. Polisi walijibu kuwa alihitaji kibali maalum.
“Nina haki ya kumkaribisha yeyote katika nyumba yangu. Je, Rais Ruto au Naibu wake wanapoandaa wageni Ikulu au Karen huwa wanatafuta kibali?” akauliza kwa ukali.
Bi Kihara alisema kuwa tayari amewahi kumkaribisha Rais Ruto katika boma hilo, na hakuelewa ni kwa nini sasa analengwa kwa kuwaalika watu wachache.
“Haya ni mateso ya kisiasa. Aibu kubwa. Rais ajue kuwa mimi si mfungwa. Nimemkaribisha hapa awali, sasa kwa nini wanatenda haya?” alisema.
Polisi walikuwa wameweka vizuizi vitatu vya barabarani kuelekea nyumbani kwake huku gari la polisi likiziba lango la kuingia nyumbani humo. Wageni hawakuruhusiwa kuingia.
Viongozi wa DCP walilaani kitendo hicho, wakikitaja kuwa njama ya kunyamazisha sauti za upinzani.
“Ananyanyaswa kwa kusema ukweli. Wafuasi wetu wamekuwa wakikamatwa na kukandamizwa kana kwamba ni wahalifu,” alisema Dkt William Wachira, mratibu wa chama hicho katika Bonde la Ufa.
Bw Gitau Mwangi, afisa mwingine wa DCP, alisema kuwa mbunge huyo ananyimwa heshima kama kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.
“Tutapinga vikali vitendo hivi vya kisiasa vya kuwakandamiza viongozi wa upinzani. Hili ni jaribio la kuzima uhuru wa kisiasa na haki za viongozi wetu,” aliongeza.
DCP imekuwa ikilalamikia mikutano yao kuvunjwa na polisi katika maeneo tofauti ya Kaunti ya Nakuru, huku baadhi ya viongozi wao wakitakiwa kufika mbele ya maafisa wa DCI bila sababu halali