Habari za Kitaifa

Kindiki na Murkomen wafichua Gachagua atakamatwa akirudi nchini kutoka Amerika

Na TITUS OMINDE August 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa DCP, Rigathi Gachagua anakabiliwa na hatari ya kukamatwa huku viongozi wa serikali wakitoa wito aandikishe taarifa kwa maafisa wa usalama kuhusu madai ya ugaidi aliyotoa akiwa Amerika.

Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, na Waziri wa Usalama wa ndani Kipchumba Murkomen, wamesema kuwa mara tu Gachagua atakaporejea nchini, ni lazima aeleze anachojua kuhusu madai hayo mazito ambayo wametaja kuwa tishio kwa usalama wa taifa.

Wakizungumza katika shule ya msingi ya Sitotwo, Kaunti ya Elgeyo Marakwet, wakati wa hafla ya kuwawezesha wanawake na waendesha bodaboda, viongozi hao walikosoa vikali kauli ya Gachagua kuhusu ugaidi, wakisema sio ya kizalendo na hatari kwa usalama wa kitaifa.

“Hatuna shida na Wakenya wanaotembelea mataifa ya nje, lakini ni lazima wabaki kuwa wazalendo. Serikali huja na kuondoka, lakini Kenya itabaki. Wale wanaomtusi Rais wasitumie nafasi hiyo kuhatarisha usalama wa nchi,” alisema Prof Kindiki.

Alisisitiza kuwa Gachagua lazima aandikishe taarifa mara moja akirejea, akisema kuwa kauli kama hiyo haiwezi kupuuzwa.

“Iwapo ana taarifa zozote kuhusu ugaidi, lazima awajibishwe. Hatuwezi kuchezea masuala ya usalama,” alisema.

Waziri Murkomen naye alisisitiza kuwa Gachagua anatakiwa kuwajibika kwa kauli zake.

“Tunamsubiri aandikishe taarifa kuhusu madai yake ya ugaidi. Mara tu atakapotua kutoka Amerika, ni lazima aeleze anachojua kuhusu Al-Shabaab na vitendo vingine vya kigaidi,” alisema Murkomen.

Murkomen alielezea kusikitishwa kwake na hatua ya Gachagua ‘kuanika masuala ya usalama’ hadharani katika nchi ya kigeni, akisema kuwa hilo ni jambo lisilokubalika.

Kauli za wawili hao zimeungwa mkono na viongozi wa Elgeyo Marakwet, akiwemo Mwakilishi wa Wanawake Caroline Ng’elechei, Mbunge wa Keiyo Kusini Gideon Kimaiyo, Mbunge wa Keiyo Kaskazini Adams Kipsanai, na Mbunge wa Marakwet Mashariki Kangogo Bowen.

Wakati huo huo, Prof Kindiki aliwataka Wakenya kupuuza wanaopinga rekodi ya maendeleo ya Rais William Ruto, akisema kuwa serikali ya Kenya Kwanza imefanya mengi katika kipindi kifupi cha chini ya miaka mitatu.

“Rais amefanikisha miradi mikubwa kote nchini. Wapinzani wake waseme wanaleta nini bora kwa Wakenya,” aliongeza.

Alitoa wito kwa wananchi kumpa Rais muhula wa pili ili kukamilisha na kupanua miradi ya maendeleo ya serikali.

Prof Kindiki pia alimtaja waziri Murkomen kuwa kiongozi anayefaa kuendeleza juhudi za kupambana na wizi wa mifugo na uhalifu katika bonde la Kerio.

Aliposimamia wizara hiyo, Kindiki aliongoza jitihada za kurejesha amani katika maeneo ya Baringo na Kerio Valley, na sasa anaamini msingi thabiti umewekwa kwa maendeleo.

Alibainisha kuwa serikali tayari imewekeza katika vifaa vya usalama kupitia mpango ili kuimarisha uwezo wa maafisa wa usalama.

“Amani imeanza kurejea Kerio Valley, na sasa ni wakati wa maendeleo. Serikali imejizatiti kutekeleza miradi ya barabara, maji, umeme, masoko, shule, na hospitali,” alieleza.