Jamvi La Siasa

Maridhiano ya taifa ni zaidi ya Raila, Ruto

Na  BENSON MATHEKA August 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HATUA ya Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kushirikiana katika utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa, ikiwemo utekelezaji wa Ripoti ya NADCO, imezua mjadala mkali kuhusu nia yao huku wakiacha nje wadau wengine katika maamuzi ya kitaifa.

Wachambuzi wa siasa na utawala wanasema vinara hao wanaonekana kuteka maamuzi yenye umuhimu wa kitaifa na kuacha nje viongozi wengine wenye ushawishi kisiasa, kidini na kijamii.

Wanasema hii ni mara ya pili kwa Raila na Ruto kuacha nje viongozi wenye ushawishi katika masuala nyeti ya kitaifa baada ya kuwapuuza walipounda Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kupitia makubaliano ya Machi 7, 2025, yaliyozaa kamati ya pamoja ya wanachama watano, wawili hao sasa wanaonekana kutawala maamuzi ya siasa za kitaifa na kuwaacha nje wanasiasa wenzao, viongozi wa dini, na wa mashirika ya kijamii.

“Mchakato huu ni wa watu wawili; lakini Kenya ni ya mamilioni,” alisema mdadisi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.Kamati mpya, inayoongozwa na Agnes Zani, imetwikwa jukumu la kusimamia utekelezaji wa vipengele 10 vya makubaliano ya ODM na UDA ambayo ni ya kitaifa na si vyama viwili pekee.

Hii ni pamoja na utekelezaji kamili wa ripoti ya NADCO ambalo ni zao la mchakato uliojumuisha muungano wa Azimio na Kenya Kwanza, haki ya maandamano ya amani na fidia kwa waathiriwa, mageuzi ya IEBC, vita dhidi ya ufisadi na usimamizi wa deni la taifa.

Hata hivyo, licha ya uzito wa ajenda hizi, hakuna kiongozi kutoka mashirika ya kijamii, taasisi za dini au vyama vingine vya siasa kama Wiper, KANU au DAP-K aliyeteuliwa katika kamati hiyo.“Raila na Ruto hawawezi kuunganisha taifa kwa kushirikiana wao wawili pekee, huku wengine wakiwa watazamaji. Huu ni mchakato wa maridhiano au wa kunufaisha wanasiasa wawili?” asema Dkt Gichuki

Anasema licha ya wito kutoka upinzani kuhusisha wadau wote katika uteuzi wa makamishna wa IEBC ilivyopendekezwa katika NADCO, Rais alipuuza.

“Ikiwa walipuuza wadau muhimu katika uundaji wa IEBC, ambayo ni moja ya mapendekezo ya NADCO, watawezaje kuthibitishia Wakenya kwamba wao wawili wanaweza kuamulia nchi mkondo faafu?” ahoji Gichuki.

IEBC ndiyo moyo wa uchaguzi na ni nguzo ya demokrasia. Kulingana na upinzani, uteuzi wa makamishna wapya ulifanywa kwa njia fiche, bila kuwahusisha wadau wote.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, ambaye alikuwa mwenyekiti mwenza wa kamati ya NADCO, sasa anaonekana kutengwa katika utekelezaji wa mapendekezo aliyoyasimamia.

Licha ya sura ya maridhiano na mshikamano inayopakwa kwenye ushirikiano wa UDA na ODM, wachambuzi wengi wasema mchakato huu hauwezi kuitwa wa kitaifa iwapo makundi muhimu yameachwa nje.Mnamo Ijumaa, viongozi hao wawili walisema kuwa hawatengani hivi karibuni, wakisisitiza kuwa ushirikiano wao unalenga kuleta utulivu na ustawi wa kiuchumi kwa wananchi.

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanahoji nia yao ya kuwaacha nje wadau wengine katika maamuzi muhimu kwa mustakabali wa nchi iwapo lengo lao ni kuunganisha taifa.

“Wanaonekana kufanya kinyume na wanachosema. Ikiwa wanatekeleza ripoti ya NADCO kwa roho safi, mbona wanaacha nje wadau wengine,” ahoji mchanganuzi wa siasa Peter Katana.

Rais Ruto na Bw Odinga walianza rasmi kushirikiana Machi 2025 waliposaini makubaliano (MoU) kwa kile wanachosema ni kuimarisha mshikamano wa kitaifa,na kushughulikia changamoto za kijamii, kisiasa na kiuchumi.