Katika ugavi wa mali ya marehemu watoto wote wana haki sawa
Sheria ya Urithi ya Kenya inasimamia ugavi wa mali ya mtu baada ya kufariki.
Sheria hii inalenga kuhakikisha kuwa watoto wote – wawe wamezaliwa ndani au nje ya ndoa – wanapewa haki sawa ya kurithi.
Katika makala hii tutaangazia vipengele muhimu kuhusu haki za watoto katika urithi, ikiwemo nani anayetambuliwa kama mtoto, iwapo watoto wanapaswa kugawana mali kwa usawa, haki za wajukuu ikiwa mzazi wao alitangulia kufariki, na kama jinsia ya mtoto ina umuhimu.
Kulingana na Sheria ya Urithi, “mtoto” ni mtoto wa kuzaliwa au wa kuasiliwa, awe mvulana au msichana, wa marehemu.
Hii inajumuisha watoto wa ndoa, watoto waliozaliwa nje ya ndoa, watoto waliotambuliwa au kukubaliwa na mwanaume kuwa wake, na hata watoto ambao huwa hawajazaliwa wakati wa kifo cha mzazi iwapo mimba ni ya marehemu.
Pia, watoto wa kambo na wale walioasiliwa na marehemu wanahesabiwa kuwa watoto halali kisheria wakati wa urithi wa mali.
Sheria inatambua umuhimu wa kuhakikisha haki sawa kwa watoto wote, bila kujali mazingira ya kuzaliwa kwao, wawe ni wadogo au watu wazima.
Ingawa sheria inapendelea ugavi sawa wa mali ya marehemu kwa watoto wake, pia inazingatia haki na hali tofauti za kila mtoto.
Mahakama zina uwezo wa kutoa sehemu kubwa ya urithi kwa mtoto mmoja ikiwa kuna sababu maalum. Kwa mfano, ikiwa mtoto huyo aliishi na kumtunza mzazi hadi kifo chake.
Sheria inaruhusu mtu yeyote mwenye maslahi kuomba apewe urithi mkubwa au hata urithi wote, iwapo anaweza kuonyesha sababu za msingi.
Hata hivyo, katika hali ya kawaida, Mahakama huangalia mambo kama mahitaji ya kila mrithi, uhusiano wao na marehemu, mchango wao kwa mali ya marehemu, zawadi za awali walizopewa, au makubaliano yaliyokuwepo kabla ya kifo.
Ni muhimu kufahamu kuwa mzazi anayeandika wosia anaweza kugawa mali kwa watoto wake kwa viwango tofauti, ilimradi iwe ni ugavi wa haki.
Sheria inawaruhusu wajukuu kurithi sehemu ambayo mzazi wao angepewa kama angekuwa hai. Hii inahakikisha kwamba kizazi cha mtoto aliyefariki kinaendelea kufaidika na mali ya familia.
Katika suala la urithi, Sheria ya Urithi haitofautishi kati ya watoto wa kiume na wa kike. Sheria inazingatia usawa wa kijinsia, na inahakikisha kuwa wavulana na wasichana wanapewa haki sawa ya kurithi mali ya mzazi wao aliyefariki.