Habari

Gavana azua hasira kwa kusema hatalipa fidia za waathiriwa wa moto

Na STEPHEN ODUOR, COLLINS OMULO August 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Tana River, Dhadho Godhana, amezua ghadhabu kwa kudai kuwa hatawalipa fidia waathiriwa wa visa vya moto katika kaunti hiyo.

Msimamo wake unakuja baada ya jopo lililobuniwa kuchunguza visa hivyo kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti yake.

Gavana amesema lengo lake lilikuwa kutathmini jinsi ambavyo kaunti imejiandaa kwa visa vya moto na kubuni mpango wa muda mrefu wa kupambana na visa vitakavyotokea.

Ufafanuzi wake umewakasirisha waathiriwa wa visa vya moto ikizingatiwa wengi wao walikuwa wakitegea fidia kutoka kwa serikali hiyo ya kaunti ili wajenge maisha yao upya.

Baadhi ya waathiriwa wa visa vya moto walipoteza mali, nyumba pamoja na wanafamilia wao.

Wakati huo huo, juhudi za kupandisha hadhi Thika kuwa jiji zimeanza kushika kasi kwenye Seneti huku Gavana wa Kiambu, Kimani Wamatangi, akitetea sana mji huo uwe jiji la sita nchini.

Kamati ya Ugatuzi kwenye Seneti kupitia Mwenyekiti wake, Abass Mohamed, imeanzisha vikao kuhusu pendekezo la Thika kuwa jiji.

Bw Wamatangi alipofika mbele ya kamati hiyo, alisema Thika ni kati ya miji inayokua kwa haraka, ina sekta imara ya utengenezaji bidhaa na ni mji ambao unapanuka kwa haraka kutokana na shughuli za kilimo kushamiri maeneo ya karibu.

Gavana anadai kuwa Thika inaweza kutumia ukanda wa Afrika Mashariki na zaidi kutokana na kuzingirwa na miundomsingi imara kama Barabara Kuu ya Thika, reli na ndiyo inaweza kufungua uchumi wa kaskazini mwa Kenya.

Mji huo pia una taasisi maarufu kama Chuo Kikuu cha Mount Kenya, ambacho ni chuo kikuu kikubwa cha kibinafsi, kile cha GRETSA kinachomakinikia teknolojia, taasisi ya Thika, Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta na kile cha Zetech.

“Thika ni kitovu cha kibiashara nchini na tunaomba Seneti iidhinishe uamuzi wa Bunge la Kaunti ya Kiambu na kufanya Thika iwe jiji kuu,” akasema Bw Wamatangi.

“Leo tuna viwanda kadhaa na tukifanya Thika iwe jiji, tutakuwa tunavutia wawekezaji kadhaa katika sekta ya utengenezaji bidhaa, teknolojia na nyanja nyingine kisha tubuni nafasi za ajira,” akasema Bw Wamatangi.

Akiendelea kutetea Thika, Bw Wamatangi ambaye alihudumu kama seneta wa Kiambu kabla ya kuwa gavana, alifichua kuwa utawala wake umeanzisha miradi mingi ya maendeleo na pia kuimarisha miundomsingi kwa zaidi ya wakazi 700,000 wa Thika.

Ili mji uwe jiji lazima uwe na zaidi ya wakazi 250,000 kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kitaifa la Takwimu Nchini (KNBS).

Pia mgao kutoka serikali kuu huongezeka iwapo mji utapandishwa hadhi ili uwe jiji.

Seneta wa Marsabit ameunga mkono pendekezo la Thika kufanywa jiji akisema itasaidia kufungua kaskazini mashariki mwa Kenya kwa maendeleo zaidi na uwekezaji.

Meya wa zamani wa Thika Mumbi Ngáru ambaye ameishi Thika kwa zaidi ya miaka 45 alisema Thika ingefanywa jiji mapema na hatua hiyo inaungwa mkonon na wakazi.