Sifuna asaka faraja kwa Kalonzo baada ya kusukumwa kwa kona na ODM
BAADA ya ishara za kudorora kwa uhusiano baina yake na baadhi ya viongozi wakuu wa chama cha ODM, Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna sasa anaonekana kusaka faraja kwa Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Mnamo wikendi kinara wa ODM Raila Odinga kwenye mazishi ya Mama Phoebe Asiyo, Kaunti ya Homa Bay aliashiria kuwa ushirikiano wake na Rais William Ruto huenda ukadumu hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2027.
Bw Odinga aliwakemea vikali wanasiasa ambao wamekuwa ‘wakiimba’ wimbo wa kumtaka Rais Ruto ahudumu kwa muhula mmoja, akisema Wakenya ndio wataamua kuhusu hilo ikifika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kauli hiyo ya Bw Raila inaenda kinyume na msimamo wa Seneta Sifuna ambaye ameshikilia kuwa hawezi kamwe kuunga mkono serikali ya Rais Ruto.
Yamkini ndiyo maana Bw Sifuna ameanza kusaka faraja katika kambi ya Bw Musyoka huku akisisitiza kuwa ODM bado iko ndani ya Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya na kinara huyo wa Wiper bado ni kiongozi wake.
“Kuna watu ambao wamesahau kuwa chama cha ODM bado kiko ndani ya Muungano wa Azimio. Mimi namtambua Kalonzo kama kiongozi wangu ndani ya Azimio na pia nawatambua ndugu zangu hawa wa Wiper kama walio ndani ya Azimio,” akasema Bw Sifuna kwenye hafla moja mjini Kitui.
Japo Bw Sifuna bado anapigania kuwepo kwa Azimio la Umoja, muungano huo unaonekana kusambaratika huku siasa za 2027 zikishika kasi.
Bw Musyoka amekuwa akishirikiana katika siasa za upinzani na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, mwenzake wa PLP Martha Karua, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi.
Bi Karua hata tayari aliondoa chama chake cha NARC-Kenya (sasa PLP) ndani ya Azimio la Umoja, baada ya mrengo wa ODM kuanzisha ushirikiano na Rais Ruto mnamo Juni mwaka jana.
Chama cha Jubilee nacho kinaonekana kutomakinikia muungano huo tena baada ya Katibu wake Mkuu Jeremiah Kioni kunukuliwa akisema watamuunga mkono Dkt Matiang’i mnamo 2027.
Kauli ya Bw Sifuna inajiri wakati ambapo anaonekana kuwa yuko guu moja nje ya ODM baada ya wandani wa Raila kusisitiza hawaondoki serikalini kiasi cha kuwa radhi kumuunga mkono Rais Ruto achaguliwe tena mnamo 2027.
Wiki moja iliyopita, Bw Sifuna alisema kuwa hatatia saini stakabadhi yoyote kati ya ODM na UDA ya kupisha Rais Ruto kuchaguliwa kwa muhula wa pili.
Bw Sifuna pia alitangaza kujiunga na mrengo mpya wa Kenya Moja ambao unawashirikisha wanasiasa chipukizi kutoka mirengo yote ya kisiasa nchini watakaokuwa wakishiriki michango ya kuinua makundi ya akinamama na vijana maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya siasa Javas Bigambo, ni dhahiri wandani wa Raila wamefaulu kumlemea Bw Sifuna ndani ya ODM na sasa lazima asake njia nyingine ya kujinusuru kisiasa.
“ODM ndiyo ilikuwa inampa Sifuna jina na anaonekana kulemewa hasa baada ya kauli ya Raila ikionyesha sasa msimamo wake wa kupinga Serikali Jumuishi hauna mashiko tena. Atapata ugumu sana kupenya kwenye siasa za jiji ikizingatiwa Raila ana ushawishi mkubwa katika siasa za Nairobi,” akasema Bw Bigambo.
Duru zinaarifu kuwa Bw Sifuna anapanga kuwania kiti cha ubunge cha Westlands, Nairobi mnamo 2027 baada ya Tim Wanyonyi kuhamisha siasa zake hadi Bungoma anakolenga kiti cha ugavana.