Habari za Kitaifa

Zogo la Gachagua na Bunge kuhusu majaji walioruhusu Kindiki kuapishwa wafika Korti ya Juu

Na JOSEPH WANGUI August 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ameitaka Mahakama ya Juu kutupilia mbali ombi lililowasilishwa na Bunge mbele yake kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu hakuwa na mamlaka ya kuteua majaji wa kusikiliza kesi ya kupinga kutimuliwa kwake (Gachagua).

Bw Gachagua aliwasilisha pingamizi hilo baada ya bunge hilo kuwasilisha rufaa katika mahakama hiyo, likitaka ibatilishe uamuzi uliotolewa Mei 2025 na mahahakama ya rufaa.

Kwenye stakabadhi alizowasilisha katika Mahakama ya Juu, Bw Gachagua anadai Bunge la Kitaifa linapania kuhujumu mamlaka ya Idara ya Mahakama na hadhi ya Mahakama ya Juu inayolindwa na Katiba.

Kulingana na mawakili wake, Dudley Ochiel na Kamotho Njomo, Bw Gachagua anasema Bunge limewasili kushikilia msimamo huo kwamba naibu jaji mkuu hana mamlaka ya kuteua jopo la majaji kusikiza kesi chini ya kipengele cha 165(4) cha Katiba.

Walisema 2021, mahakama ilikubaliana na ombi la Bunge, katika kesi tofauti kuhusu kuvunjwa kwake kwa kutopitisha sheria ya usawa wa kijinsia kwa misingi ya hitilafu katika uteuzi wa majaji wa kusikiza kesi.

“Sheria hairuhusu wahusika katika kesi kuibua misimamo tafauti kuhusu kesi inayofanana.”

Bunge la kitaifa halifai kuchukua msimamo tofauti kuhusu suala lililoko chini ya kipengele cha 165 (4) cha Katiba,” mawakili hao wakaeleza.