Habari

Polisi wasema watapekua kila mahali kubaini kiini cha ajali zilizoua 60 ndani ya siku tatu

Na CHARLES WASONGA August 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HUDUMA ya Kitaifa ya Polisi (NPS) imeanzisha uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ongezeko la ajali za barabarani zilizoshuhudiwa maeneo mbalimbali nchini katika siku chache zilizopita.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumapili, Agosti 10, 2025, msemaji wa huduma hiyo Muchiri Nyaga alisema polisi wanashirikiana na maafisa kutoka asasi zingine katika uchunguzi huo.

NPS imetangaza hatua hiyo baada ya karibu watu 60 kufa katika ajali za barabarani nchini ndani ya muda wa saa 72 (siku tatu) pekee.

Ajali za hivi punde ni ile iliyohusisha basi la kampuni ya Ena Coach Jumamosi usiku katika barabara ya Mai Mahiu-Narok ambapo watu wawili walikufa.

“Katika siku chache zilizopita, tumeshuhudia msururu wa ajali za barabara sehemu mbalimbali nchini. Kwa hivyo, Huduma ya Kitaifa ya Polisi inashirikiana na asasi mbalimbali za serikali kuendesha uchunguzi wa kina kwa lengo la kubaini kiini cha ajali hizi,” Bw Nyaga akasema.

“Ajali za barabara huathiri familia pakubwa na hatua zote zinapasa kuchukuliwa kuzuia maafa zaidi. NPS inatoa rambirambi zake kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwatakia afueni ya haraka wale wanaouguza majeraha hospitalini,” akaongeza.

Kulingana na Bw Nyaga ajali hizo zinaweza kuzuiwa ikiwa waendeshaji magari watazingatia sheria za trafiki, kukoma kuendesha kwa kasi zaidi, miongoni mwa kanuni zingine za usalama barabarani.

NPS imeshauri abiri kutoa ripoti kuhusu madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani kwa nambari zisizolipiwa za 999, 911, hashtegi #Fichuakwa DCI, nambari ya WhatsApp 0709 570 000 au nambari 08 722 203 ambayo haitozwi pesa zozote.

Mnamo Ijumaa Agosti 8, 2025, watu 26 kutoka familia moja waliangamia katika ajali mbaya iliyotokea katika mzunguko wa barabara ya Coptic katika barabara ya Kisumu-Kakamega.

Hii ni baada ya basi la shule ya Upili ya AIC Naki iliyobeba watu 60 waombelezaji walitoka eneo la Nyahera kuanguka.