Habari

Wabunge wajipata matatani wakazi wakiwazomea kuhusu SHA

Na GEORGE MUNENE August 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKAZI wa Mwea wamelalamikia dhuluma kali ambayo wamewekewa wakisaka huduma kupitia Bima ya Afya ya Kijamii (SHA) ambapo sasa wasioajiriwa wanatakiwa kulipia kwa mwaka ili kupata huduma za afya.

Wabunge watano wanaogemea mrengo wa serikali walikuwa na wakati mgumu kuwakabili wakazi ambao walikuwa wakilalamikia hitaji la kulipia SHA kwa mwaka.

Wakiongea katika Shule ya Mseto ya Ngurubani eneobunge la Mwea, wakati wa mchango wa kuwapiga jeki makundi ya akina mama kifedha, wakazi waliwaambia wabunge hao kuwa hawana fedha za kulipia SHA kila mwaka na walikuwa wakiteseka kugharimia matibabu yao wenyewe.

Wabunge waliohudhuria mchango huo walikuwa Mwangi Kiunjuri (Laikipia Mashariki), Gachoki Gitari (Kirinyaga ya Kati), Mary Maingi (Mwea), Dorothy Muthoni (Mteule) na Jane Kagiri (Mbunge Mwakilishi wa Kike).

“Serikali inafaa ituruhusu kulipa SHA kila mwezi ili tupokee huduma za kimatibabu jinsi ambavyo ilikuwa wakati wa NHIF,” akasema mmoja wa wakazi.

Wengi walilalamika kuwa gharama ya juu ya maisha imesababisha wasiweze kulipa kila mwaka.

Bw Kiunjuri aliwaambia amesikia kilio chao na atakifikisha kwa serikali ili baadhi ya Wakenya wasihisi wametengwa kwenye matumizi ya SHA.

Bi Muthoni alisema kuwa Rais William Ruto anastahili kuambiwa kuwa Wakenya wanatesekea SHA na wanahitaji kupata huduma za kimatibabu bila kutaabika.

Wabunge hao waliwaambia wakazi kutoka Mlima Kenya wapuuze upinzani na washirikiane na serikali katika kutimiza ajenda kwa Wakenya.