Nimewaona pamoja na wanasoma chuo kimoja; nagongewa msupa au ni marafiki tu?
Mpenzi wangu anasoma chuo kikuu. Kuna jamaa nimewaona pamoja mara kadhaa na siku fulani nilimpata kwake. Nimemuuliza akasema wanasoma pamoja. Inawezekana ananicheza?
Mwanawake na mwanamume wanaweza kutangamana bila uhusiano wa kimapenzi. Lakini pia ushirikiano huo unaweza kuzaa mapenzi. Huna sababu ya kumshuku mpenzi wako, lakini ni muhimu ufuatilie kwa karibu mienendo yao.
Aliniweka presha tukala uroda sasa ninamchukia
Mpenzi wangu alinilazimisha tushiriki mapenzi na baada ya hapo nikamchukia na kumuacha. Ameniomba msamaha akitaka turudiane lakini bado nina maumivu moyoni kutokana na alichonitendea. Nifanyeje?
Mpenzi wako alifanya makosa makubwa kukulazimisha kufanya jambo ambalo hukutaka. Hatua yake ya kurudi kwako kuomba msamaha ni ishara kuwa anajuta. Kama bado unampenda, shauri moyo wako uone kama unaweza kumsamehe.
Nilipekua simu yake nikakumbana na vituko
Miezi miwili iliyopita nilipata ujumbe wa kimapenzi katika simu ya mpenzi wangu kutoka kwa mwanamke mwingine. Nimechunguza na hatimaye nimethibitisha huyo ni mpenzi wake.
Uliamua kumchunguza mpenzi wako ili ujue ukweli kuhusu uhusiano wake na mwanamke huyo kwa sababu hutaki mpenzi asiye mwaminifu. Sasa umethibitisha, utaamua mwenyewe iwapo utajiondoa ama utaendelea.
Ndoa yake ilivunjika ila nahofia mke atarudi
Huu ni mwaka wangu wa pili katika uhusiano wa kimapenzi. Nimegundua mpenzi wangu alikuwa ameoa na wakaachana na mkewe. Nahofia mke wake anaweza kurudi baadaye.
Ni kawaida kwa mtu na mkewe kuachana. Sielewi ni kwa nini mpenzi wako hakukwambia ukweli kuhusu maisha yake. Kwa sababu umejua, shauriana naye ili uhakikishe hakuna matumaini ya kurudiana ndipo muendelee na uhusiano wenu.