Habari za Kitaifa

Kalonzo anawaniwa kweli ama ni mbinu ya kujipendekeza?

Na CECIL ODONGO August 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka ameibuka mwanasiasa ambaye sasa anawaniwa na mrengo wa Rais William Ruto hatua inayoonekana kulenga kuharibu umoja wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Wikendi, Bw Musyoka pamoja na wandani wake walionekana kukiri kuwa kuna shinikizo zinazoendelea kutoka kambi ya serikali ili aasi upinzani na kujiunga na mrengo wa Rais Ruto.

Katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii, Bw Musyoka alionekana kukubali kuwa anaandamwa lakini akasisitiza kuwa hatajiunga na serikali na sasa anamakinikia safari yake ya ikulu mnamo 2027.

“Sitanunuliwa ili nijiunge na serikali na iko tayari kulipa adhabu yoyote kuhakikisha Rais Ruto anahudumu muhula mmoja. Sitawaacha Wakenya na lengo langu ni kuhakikisha Ruto anahudumu muhula mmoja,” akaandika Bw Musyoka kwenye mtandao wake wa kijamii.

Wandani wake – Seneta wa Kitui Enock Wambua na Naibu Gavana Francis Mwangangi – wameonya upande wa serikali iachane na Bw Musyoka kwa sababu watahakikisha anakuwa rais mwaka wa 2027.

“Rais wachana na Kalonzo kabisa, hii fitina mnafanya kila wakati kuwa Kalonzo anataka kujiunga na serikali yenu haitatimia. Kalonzo hatajiunga na serikali yako wakati wowote,” akasema Bw Wambua.

“Kalonzo hana nia ya kukutana na wewe na kama Wiper tumeamua siku Kalonzo atakutana na Ruto ni pale Kasarani akimpa vyombo vya mamlaka,” akaongeza Bw Wambua wakati akizindua kampeni zake za ugavana wa Kitui 2027 katika eneo la Kitui Magharibi.

Bw Mwangangi naye alijinaki kuwa Kalonzo ndiye sasa nyapara wa upinzani na kuna kila ishara atapeperusha bendera yao mnamo 2027.

“Kalonzo haendi kwa Ruto na sisi hatutafanya kazi na Ruto ila tunatafuta urais. Hatumtaki Ruto na Kalonzo haendi huko,” akasema Bw Mwangangi.

Kauli za Bw Musyoka mwenyewe na wandani wake zinafufua uvumi kuwa makamu huyo wa rais wa zamani amekuwa akifikiwa na utawala wa sasa ili kurahisisha nafasi ya Rais Ruto kushinda awamu ya pili mnamo 2027.

Bw Musyoka kwa sasa yuko kwenye muungano wa upinzani na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kinara wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, Spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Kinara wa PLP Martha Karua.

Mnamo Juni 12 akiwa katika Kaunti ya Kitui, Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki alimrai Bw Musyoka aasi upinzani akimwaahidi kuna mnofu wake ndani ya serikali ya Kenya Kwanza.

“Nimeona watu wengine wakiungana na Kalonzo na kumshawishi achukue mwelekeo wa kisiasa ambao ni wa kikabila. Binafsi nitamtafuta kwa sababu ni wakili kama mimi,” akasema Profesa Kindiki.

“Kati ya mimi na wao, nani anaweza kumpa mwelekeo wa kisiasa unaomfaa?” akauliza Profesa Kindiki aliyerithi nafasi ya Bw Gachagua mnamo Novemba 2024.