Habari

Gachagua: Raila amenyamaza anakula peke yake, atakumbuka wafuasi uchaguzi ukifika

Na CECIL ODONGO August 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa ODM Raila Odinga ‘amefikiwa’ na matamshi makali ya Rigathi Gachagua baada ya aliyekuwa naibu rais kudai kwamba huwa hataki kuwa rais katika kila uchaguzi.

Kwenye matamshi makali ambayo yanatarajiwa kuchemsha uongozi wa ODM, Bw Gachagua amesema Raila huwania urais bila kutaka wadhifa huo.

Anadai Raila anataka mamlaka bila uwajibikaji ndiposa amekuwa akiwahadaa wafuasi wake wamfuate lakini akifika debeni anahakikisha ameshindwa kwa kutumia mbinu zote.

“Kila uchaguzi Raila amekuwa akiwatumia binamu kutoka Ukambani, Mulembe, Taita, Kisii, Mijikenda na anawadanganya anawapeleka Canaan.”

“Kwa sababu binamu wanataka kuingia huko wanamfuata. Akiingia huko hataki kuwa rais, anataka tu mamlaka bila uwajibikaji. Anazua ghasia ili ajiunge na serikali kisha anaanza kula na kunyamaza akisubiri uchaguzi mwingine kuwahadaa tena,” akaongeza Bw Gachagua.

Alikuwa akizungumza Amerika ambako amekuwa akiendeleza ziara ya miezi miwili ya kukutana na Wakenya ambao wako huko.

Aliyekuwa naibu rais alisisitiza kuwa siasa za Raila zimeisha na kazi yake ni ‘kula serikalini’ akiwa amenyamaza.

“Sasa amenyamaza kwa sababu yupo mezani anakula. Binamu nao wamemtoroka na wanazungumza lugha moja. Raila alikuwa akilia kwenye mazishi ya Phoebe Asiyo si kwa sababu alikuwa akimwomboleza marehemu bali alikuwa akiwalilia binamu aliowapoteza,” akasema Bw Gachagua.

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira alimtaka Raila kusahau kupata uungwaji mkono wa ‘cousins’ kwa sababu alienda kwa Rais Ruto na kuanza kula pekee yake.

“Hii ni mambo ya familia (vuguvugu la cousins) na Raila asiingilie. Sote kwa sasa tunazungumza lugha moja na Raila hana nafasi tena ya kututumia kusaka urais ambao hautaki,” akasema.

Kauli ya Bw Gachagua inakuja wakati uhusiano kati ya Raila na Rais Ruto umeonekana kunoga kuelekea kura ya 2027.

Ijumaa iliyopita, Raila aliwakemea vikali wale ambao wanasema Rais Ruto anastahili kuhudumu kwa muhula moja pekee, akisema hiyo itaamuliwa na Wakenya kutokana na utendakazi na uwajibikaji wa serikali ya sasa.

Tangu aingie Amerika, Bw Gachagua amekuwa akirusha kila aina ya bomu. Wiki jana, alisema yuko tayari kusaidia Amerika kuanza kuchunguza maovu ya utawala wa Rais Ruto.

Alidai kuwa ana habari fiche kuhusu jinsi Rais anavyoshirikiana na magaidi na kufadhili kundi la wapiganaji wa RSF ili kuhakikisha Sudan haina udhabiti.