Serikali yaanza ukaguzi wa barabara kubaini sehemu zilizo na kasoro
JUMLA ya watu 80 wamekufa katika ajali za barabarani ndani ya siku nne zilizopita huku serikali ikianzisha ukaguzi wa barabara mbalimbali kubaini sehemu zilizo na kasoro.
Aidha, jumla ya watu 2,933 wamepoteza maisha yao kwenye ajali hizo kati ya Januari 1, 2025 na Agosti 10, kulingana na taarifa iliyotolewa na Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir Jumatatu jioni.
“Takwimu za ajali zinaonyesha kuwa jumla ya watu 2,933 wamepoteza maisha yao katika barabara za humu nchini kati ya Januari na Agosti 10, 2025. Inasikitisha kuwa vifo 80 vilitokea ndani ya siku nne zilizopita,” akasema.
“Kufuatia ongezeko la ajali zinazohusisha magari ya umma, magari ya kibinafsi na yale ya kibiashara, maafisa kutoka asasi mbalimbali za serikali wanaendesha ukaguzi wa kiusalama katika sehemu husika za barabara kutambua dosari ili kupendekeza marekebisho yanayopaswa kufanywa,” Bw Chirchir akaongeza.
Waziri alisema kikosi hicho kitakamilisha zoezi hili ndani ya siku saba zijazo na kuwasilisha mapendekezo kuhusu hatua za kiufundi zinazopasa kuchukuliwa kuzuia maafa.
Bw Chirchir alisema serikali inajitolea kutekeleza mikakati ya usalama iliyoorodheshwa katika Mpango wa Kitaifa wa Usalama Barabarani wa 2024-2028.
“Tutaendelea kushirikiana na wadau wote katika kufanikisha utekelezaji wa mikakati yote ya usalama barabarani iliyomo kwenye stakabadhi hiyo,” akaeleza.
Baadhi ya mikakati hiyo inahusu mageuzi ya kanuni kuhusu matumizi ya magari ya shule, shughuli za magari ya kusafirisha bidhaa na mafuta, kudhibitiwa kwa mienendo ya madereva kuendesha wakiwa walevi, ukaguzi wa magari na mageuzi kwa Sheria za Trafiki.
Bw Chirchir pia ametaja utekelezaji wa miradi ya serikali inayolenga kuimarisha usalama barabarani.
Mifano ni; ujenzi upya wa Daraja la Nithi, katika kaunti ya Tharaka Nithi na mradi wa upanuzi wa barabara ya Rironi-Mau Summit unaotarajiwa kuanzia Oktoba mwaka huu.
Bw Chirchir alisema Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA) itaimarisha ushirikishi wa shughuli za udumishaji usalama na uhamasisho wa umma kuhusu haja uzingatiaji wa sheria za barabarani.
“Wizara yangu inatoa wito kwa wadau wote katika uchukuzi wakiwemo madereva, watembeaji kwa miguu, wahudumu wa boda boda na waendesha baiskeli kulinda usalama usalama wao,” akaeleza.
Ajali ya hivi punde ilitokea Jumatatu jioni katika barabara ya Kisumu-Busia na kuhusisha basi la kampuni ya Royal Liner lililogongwa na trela katika eneo la Lela, karibu na Maseno.