Habari za Kitaifa

Mwambieni Ruto nimejiunga na ‘Wantam’, wilbaro yake imetoboka huku Gusii – Machogu

Na WYCLIFFE NYABERI August 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amedokeza sababu zilizopelekea kufutwa kwake kutoka serikalini.

Bw Machogu, ambaye aliwania bila mafanikio kiti cha ugavana wa Kisii katika uchaguzi mkuu wa 2022, alikuwa miongoni mwa mawaziri ambao hawakurudishwa kazini kufuatia maandamano ya vijana wa Gen Z, waliokuwa wakilalamikia uongozi mbaya.

Maandamano hayo yalifanyika Juni mwaka jana na kukolea zaidi mwezi Julai.

Baada ya kufyata ulimi kwa muda wa mwaka mmoja tangu kufurushwa kwake, mbunge huyo wa zamani wa Nyaribari Masaba amedai alichochewa kufutwa na kwa Rais William Ruto.

Akizungumza Jumatatu alipohudhuria mazishi ya Esther Kemunto — mamake aliyekuwa Mbunge wa Nyaribari Chache Richard Nyagaka Tong’i katika Kijiji cha Amariba, Bw Machogu aliapa kulipiza kisasi dhidi ya wabunge hao kwa kumchongea alipokuwa waziri.

Katika mazishi mengine wiki jana katika Kaunti ya Nyamira, waziri huyo wa zamani alidai kuwa wabunge hao walitaka upendeleo kutoka kwake alipokuwa akiongoza wizara hiyo inayopewa bajeti kubwa lakini akakataa.

Aliyekuwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu akihutubu katika mazishi ya Esther Kemunto- mamaye mbunge wa zamani wa Nyaribari Chache Richard Tong’i, Nyaribari Chache, Kisii, Agosti 11, 2025. Picha|Wycliffe Nyaberi

“Wakati nilikuwa ninaongoza Wizara ya Elimu, baadhi ya wabunge kutoka eneo hili, walinitafuta wakitaka niwape zabuni kwa njia zisizofaa wizarani. Kama mjuavyo, Machogu hapendi njia za mkato na niliwaambia wafuate utaratibu unaostahili.  Hawakufurahishwa na hilo na hapo ndipo walipopanga njama ya fitina na kampeni ya kuhakikisha nimetimuliwa kutoka kwenye baraza la mawaziri,” Bw Machogu alisema Ijumaa wiki jana katika Shule ya Msingi ya Menyenya, wakati wa mazishi ya Bi Catherine Nyamato, ambaye alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka jamii ya Abagusii kuteuliwa bunge la kitaifa.

Alimtaja Rais William Ruto kuwa mwongo na akawataka wandani wake wa Kisii kumpelekea ripoti kuwa amejiunga rasmi na kikosi cha “Wantam”.

Bw Machogu alisema siku za Rais Ruto ni za kuhesabika akisema Wakenya watamtimua katika uchaguzi mkuu ujao.

“Wilbaro haifanyi kazi tena. Imetoboka. Mimi ndiye niliyekuwa sura ya wilbaro Gusii lakini nimeondoka sasa. Wilbaro hiyo sasa imekuwa chuma chakavu,” waziri huyo wa zamani alisema.

Bw Machogu aliikashifu mipango ya serikali ya uwezeshaji wa kinamama na vijana akisema hafla hizo zinadhalilisha makundi hayo kutokana na viwango vyao vya chini vya mapato yao.

Kutoka kushoto: Aliyekuwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, Innocent Obiri (Mbunge wa Bobasi), Naibu Gavana wa Kisii Elijah Obebo na Mbunge wa Nyaribari Chache Zaheer Jhanda wafuatilia matukio katika mazishi ya Esther Kemunto -mamake aliyekuwa Mbunge wa Nyaribari Chache Richard Tong’i katika kijiji cha Amariba, Kaunti ya Kisii mnamo Agosti 11, 2025. Machogu amesema amejiunga rasmi na vuguvugu la “Wantam” na kuongeza kuwa chama tawala cha UDA Gusii sasa ni gofu. Picha|Wycliffe Nyaberi

“Tulipokuwa tunawaambia tunawainua kutoka chini kwenda juu, tulikuwa tunamaanisha tuchukue pesa za serikali na kuwaletea? Kwani nyinyi ni watu wenye thamani ya Sh64 kila moja? Hiyo ni kama kuwatapikia,” Bw Machogu aliambia wakazi wa Nyamira.

Aliitaka jamii ya Abagusii kuungana nyuma ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i, ambaye ametangaza nia yake ya kuwania urais 2027.

“Sasa tuna mwana wetu Dkt Fred Matiang’i. Tafadhali sote tuungane nyuma yake. Hatutarudia makosa tuliyofanya tena. Tumeungana na hata Profesa Sam Ongeri na tunataka kuanza kuunganisha watu wetu,” Bw Machogu alisema.