Habari za Kitaifa

Ruto mbioni kunasa Gen Z ambao wamekuwa wakipinga serikali yake

Na SHABAN MAKOKHA August 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto sasa amegeukia vijana – ambao wamekuwa wakipinga serikali yake akijaribu kuwavutia kwa ahadi za ajira, fursa za biashara, mitaji na juhudi za kuwainua kiuchumi na kijamii.

Katika jitihada za kuvutia uungwaji mkono wa vijana kuelekea uchaguzi wa 2027, Rais alitangaza kuwa serikali inatekeleza mikakati kabambe ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana tatizo linalowakumba maelfu ya vijana Wakenya wanaokabiliana na hali ngumu za maisha.

Akihutubia maelfu ya vijana katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana yaliyofanyika Kaunti ya Kakamega siku ya Jumanne, Rais alisema taifa halijawahi kuwa na mpango makusudi wa kuwapatia vijana ajira kwa miaka mingi.

Alitaja miradi kadhaa inayotekelezwa na serikali yake kwa ajili ya vijana ikiwemo: mradi wa Nyumba Nafuu, ajira nje ya nchi, uchumi wa kidijitali, Kazi Mtaani, ufadhili wa biashara na mikopo kwa vijana.

“Kama serikali, tunajali kizazi kijacho. Tuna mipango ya kuwaelimisha, kuwapa mafunzo, ufadhili, na ushauri. Tusikubali waingie katika uraibu wa dawa za kulevya au kunaswa na wanasiasa wanaotaka kuwatumia kwa maslahi yao binafsi,” alisema Rais Ruto.

Kauli hiyo inajiri kufuatia uhusiano uliodorora kati ya Rais na kizazi kipya cha vijana wa Gen Z, kufuatia hali ngumu ya kiuchumi, ukosefu wa ajira, na miswada tata ambayo ilizua maandamano makubwa nchini.

Vijana hao waliandaa maandamano ya aina yake wakipinga Mswada wa Fedha 2024, ongezeko la ushuru, na ukatili wa polisi.

Walitaka uongozi bora, utawala wa sheria, usawa wa kijamii, na maadili katika uongozi wa umma.

Ingawa serikali ilisema maandamano hayo yalichochewa kisiasa, wachambuzi walisema ilikuwa ishara ya mgogoro mkubwa wa uhalali wa uongozi, na wakasisitiza haja ya mazungumzo ya maana kati ya serikali na vijana.

Akiwahutubia viongozi wa vijana kutoka kaunti zote 47, Rais Ruto alisisitiza kuwa katiba inaitaka serikali kuwekeza kwa vijana kwa kuwapa elimu, mafunzo, na fursa zinazolingana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya ajira.

“Katiba yetu inatutaka tuwasaidie vijana wetu. Wao si viongozi wa kesho tu – bali ni wa leo na wabunifu wa mustakabali wetu,” alisema Rais.

“Tunajivunia vijana wetu. Wao ndio rasilmali muhimu zaidi tuliyo nayo. Wana maarifa, ubunifu na nguvu ya kuijenga Kenya mpya,” aliongeza.

Alitoa mfano wa timu ya kitaifa ya kandanda, Harambee Stars, kama ishara ya uwezo na ubunifu wa vijana wa Kenya.

“Ndiyo maana nimefurahi kuwa hapa kusherehekea nguvu na ubunifu wa vijana, na kutambua mchango wao mkubwa kwa ajenda ya mageuzi ya kitaifa,” alisema.

Rais alizindua mpango wa National Youth Opportunities Towards Advancement (NYOTA) unaolenga kuwasaidia zaidi ya vijana 100,000 nchini kwa kuwapa mafunzo, usaidizi wa biashara na ajira.

Katika awamu ya kwanza, vijana 90,000 wenye umri wa miaka 19–29 waliomaliza kidato cha nne lakini hawana ujuzi maalum watapatiwa mafunzo ya stadi muhimu na marupurupu kwa kipindi cha mwaka mmoja. Kisha wataunganishwa na waajiri kwa nafasi za mafunzo kwa vitendo, huku serikali ikifanikisha mchakato wa uajiri wao.

Kupitia mpango wa kuendeleza biashara ndogo, serikali inalenga kuwachagua vijana 70 kutoka kila wadi kufikia Septemba 2025, kuwapa mafunzo na kisha kuwakabidhi Sh50,000 kila mmoja kama mtaji wa kuanzisha biashara ndogo kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kijamii na kuunda ajira.

Rais pia alitangaza kuwa vijana 600,000 watanufaika kupitia mpango ambao utawasaidia kupata zabuni za serikali, kushiriki kwenye masoko mtandaoni na kufaidika na ufadhili wa Sh1 bilioni.

Katika hafla hiyo, Rais alipatia vijana hundi ya Sh163 milioni kusaidia vijana 816 waliopata ajira nje.

Kwa mujibu wa Rais, vijana 420,000 tayari wamepata ajira nje ya nchi katika kipindi cha miaka miwili na nusu kupitia mpango wa Kazi Majuu, unaoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Kenya na mataifa kama Ujerumani na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Dkt Ruto alisema lengo la miradi hiyo ni kupunguza ukosefu wa ajira na kukuza ujasiriamali miongoni mwa vijana nchini.

Alizindua pia tovuti ya ‘Kuna Form’, ambayo itarahisisha upatikanaji wa fursa za biashara kwa vijana kupitia serikali.

Rais alisema kuwa mradi wa zamani wa Kazi kwa Vijana sasa umebadilishwa kuwa Climate Works, ambao tayari umeanzishwa Nairobi.

“Tutaupanua mpango huu nchi nzima kupitia mradi wa barabara, ambapo vijana 113,000 watanufaika – wakiwemo 4,000 kutoka Kaunti ya Kakamega,” aliongeza.

Waliomwandamana rais walikuwa ni Waziri wa Vijana, Uchumi wa Ubunifu na Michezo Salim Mvurya, na Waziri wa Maendeleo ya Ushirika na Biashara Ndogo Wycliffe Oparanya.

Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa alimsifu Rais Ruto kwa juhudi zake za kuwawezesha vijana na kusaidia miradi mikuu ya maendeleo katika kaunti hiyo.

“Nashukuru pia serikali kwa kusaidia miradi mikubwa kama upanuzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kakamega na ujenzi wa uwanja wa Bukhungu kwa viwango vya kimataifa,” alisema Bw Barasa.