Habari

Mkosi wa kwanza? IEBC yaambiwa imehesabu vibaya tarehe ya chaguzi ndogo

Na DAVID MWERE August 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UAMUZI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza Novemba 27, 2025 kuwa siku ya chaguzi ndogo umetajwa na wanasheria na wanasiasa mashuhuri kuwa kinyume cha Katiba, huku wakionya kwamba hatua hiyo inaweza kufungua milango ya kesi mahakamani au hata amri ya kuzuia uchaguzi huo.

Tume hiyo, inayoongozwa na mwenyekiti mpya Bw Erastus Ethekon Edung, imeanza kazi kwa lawama kali, huku wengi wakihofia kuwa huenda ikazua migogoro ya kisheria badala ya kutekeleza majukumu yake kwa kufuata katiba.

Kupitia notisi ya serikali ya Agosti 8, 2025, Bw Ethekon alitangaza rasmi kuwa uchaguzi huo mdogo utafanyika Novemba 27, ukihitimisha kipindi cha kusubiri kwa muda mrefu kwa wananchi waliopoteza wawakilishi wao.

Hata hivyo, kuhesabu siku 90 kutoka tarehe ya kutangazwa kwa nafasi wazi kunamaliza kipindi hicho mapema zaidi na hivyo kufanya tarehe ya uchaguzi huo iwe nje ya muda uliowekwa na Katiba.

Kifungu cha 101(4)(b) cha Katiba kinaitaka IEBC kufanya uchaguzi mdogo ndani ya siku 90 baada ya viti kutangazwa kuwa wazi kupitia ilani kutoka kwa maspika wa mabunge husika.

Mwanasheria na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna alikuwa wa kwanza kuikosoa IEBC.

“Katiba iko wazi kuwa uchaguzi mdogo uandaliwe ndani ya siku 90 baada ya nafasi kuwa wazi. Lakini tume hii imeanza vibaya kwa kuvunja sheria ya wazi kabisa,” alisema Seneta huyo.

Bw Sifuna pia aliikashifu tume hiyo kwa kushindwa kufuata sheria wakati wa kuchagua mrithi wa aliyekuwa Mbunge Maalum John Mbadi, aliyeteuliwa kuwa Waziri.

Alisema Mbadi aliteuliwa kupitia kundi la wafanyakazi, lakini tume haikuheshimu muktadha huo.

Wakili mashuhuri Charles Kanjama alisema kwamba kutokana na IEBC kuchelewa kuundwa, muda wa siku 90 tayari umepita na hivyo tarehe ya Novemba 27 inafaa.

Lakini kauli hiyo ilipingwa vikali na waliokuwa maafisa wa juu serikalini, wakiwemo Mwanasheria Mkuu wa zamani Justin Muturi, Wakili Kibe Mungai, Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jr, Seneta wa Makueni Daniel Maanzo, na Wakili David Ochami.

“Haiwezekani tume iliyoundwa kwa msingi wa kuheshimu sheria ianze kwa kuvunja Katiba. Wanaonekana hawajui hata walivyoamua tarehe hiyo,” wakili Mungai aliongeza: “Huu ni mpango wa kuchelewesha kesi za kuwaondoa wabunge waliopo. Tunawaona kutoka mbali.”

Wengine walionya kuwa ukiukaji huu unaweza kufungua mlango wa kesi nyingi dhidi ya IEBC, hali itakayopelekea matumizi mabaya ya fedha za umma katika kujitetea mahakamani.

Naye Gavana Mutula alisema: “Katiba haisihi. Muda wa uchaguzi haubadilishwi. Wakiruhusu hili dogo leo, kesho uchaguzi wa rais utacheleweshwa kwa siku 15. Hawako sahihi.”

Wakili Ochami naye alisema IEBC ilipaswa kuomba ushauri rasmi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu kabla ya kutoa tarehe hiyo tata.

“Wangeeleza hadharani jinsi walivyohesabu muda wa siku 90. Kukosa uwazi ni mwanya wa matumizi mabaya ya rasilimali za umma,” alisema.

Seneta Maanzo alionya kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha mchakato mzima wa uchaguzi huo kutangazwa kuwa batili mahakamani.

Maeneo ambako uchaguzi mdogo unasubiriwa ni Kaunti ya Baringo (Seneti) – kufuatia kifo cha aliyekuwa seneta William Cheptumo mnamo Februari 16, 2025, Banissa, baada ya Mbunge Hassan Kullow kufariki katika ajali mnamo Machi 29, 2023, Magarini baada ya Mahakama kuidhinisha kufutiliwa mbali kwa ushindi wa Bw Harrison Kombe mnamo Mei 31, 2024, Ugunja baada ya aliyekuwa Mbunge Opiyo Wandayi kuteuliwa kuwa waziri mnamo Agosti 8, 2024.

Mengine ni Malava baada ya Mbunge Malulu Injendi kufariki dunia mnamo Februari 17, 2025,Mbeere Kaskazini baada ya Geoffrey Ruku kuteuliwa kuwa Waziri mnamo Aprili 17, 2025 na Tume ya IEBC bado haijatoa maelezo ya kina kuhusu ni kwa nini haikuheshimu kipindi cha siku 90 kama ilivyoainishwa na Katiba.