Habari za Kitaifa

Ukora: Skendo ya tiketi za CHAN yagharimu Kenya faini kubwa, kukosesha mashabiki mechi

Na TOTO AREGE August 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUFIKIA Julai 28, siku saba kabla ya mechi ya ufunguzi ya kinyang’anyiro cha Kombe la Ubingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Nyumbani (CHAN), kati ya Harambee Stars na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), tovuti ya tiketi ilionyesha kuwa tiketi za mechi hiyo zilikuwa zimeisha.

Hii ilikuwa habari njema, kwani ilimaanisha kuwa Stars ingekabiliana na mabingwa hao mara mbili wa CHAN mbele ya mashabiki wengi katika Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani (MISC), Nairobi ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 48,000 na zaidi.

Kabla ya mechi hiyo muhimu, kulikuwa na madai kutoka kwa Wakenya kadhaa mtandaoni kwamba viongozi wakuu serikalini walikuwa wamenunua tiketi hizo ili kuwapa watu wanaounga mkono serikali ya Kenya Kwanza.

Baadhi yao walidai kuwa hatua hiyo ililenga kukabiliana na uwezekano wa matamshi ya kupinga serikali wakati wa mechi hiyo kama vile “wantam”.

Madai hayo yalienea baada ya video kuibuka zikionyesha sehemu ya wanasiasa wanaohusishwa na serikali wakionyesha tiketi za kadi mitandaoni.

Lakini akizungumza katika kipindi cha asubuhi katika runinga ya NTV wakati wa kipindi cha Fixing The Nation Jumatatu iliyofuatia, mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kenya (LOC) Nicholas Musonye alikanusha madai ya ununuaji wa tiketi nyingi kwa wakati mmoja na watu mashuhuri serikalini.

“Hili suala halipo,” alisema Musonye.

Katika mechi iliyofuatia baina ya Kenya na Angola mnamo Alhamisi iliyopita, mashabiki 46,520 waliingia Kasarani. Siku tatu kuelekea mechi hiyo, tiketi zote 48,000 zilikuwa zimeuzwa pamoja na mechi ya Morocco.

Idadi kamili ya mshabiki waliohudhuria mechi ya Morocco haikutangazwa.

Uchunguzi wetu ulibaini kwamba, tiketi 25,000 ziliwafanyiwa skani lakini zaidi ya mashabiki 75,000 walihudhuria mechi hiyo.

Mashabiki walisukumana kwenye malango ya uwanja wa Kasarani na hata kuyavunja kabla ya kuingia ndani.

Kutokana na hali hiyo mnamo Jumanne Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lililipa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) adhabu kali kwa kupunguza idadi ya mashabiki watakaohudhuria mechi ya mwisho ya Kundi A kutoka 48,000 hadi 27,000 (kupungua kwa asilimia 40).

Haya yalijiri wiki moja tu baada ya kamati ya nidhamu ya CAF kuipiga FKF faini ya Sh 2.5 millioni kutokana na ukiukaji wa Kanuni za Nidhamu za CAF, pamoja na Kanuni za Usalama wakati wa mechi mbili za kwanza za hatua ya makundi.

Tovuti ya kununua tiketi ya mechi ijayo ilifunguliwa usiku wa manane kuamkia jana na chini ya masaa manne, tiketi zote 27,000 zilikuwa zimeisha.

Kabla ya kufunguliwa, FKF ilipewa onyo kali na CAF iliyopiga marufuku tiketi za kadi ama karatasi na kuruhusu tiketi za elektroniki pekee wakati wa mechi ya Zambia na robo fainali.

Baadhi ya mashabiki walielezea kwamba, hata baada ya kukosa tiketi kwenye tovuti watatumia mbinu nyingine za kununua tiketi langoni Kasarani.

“Tikiti zilikuwa zikiuzwa katika barabara kuu ya Thika jijini Nairobi nje tu ya Hoteli ya Safari Park kwa Sh250,” alisema mmoja wa mashabiki, akiwa na imani kwamba, atapata tiketi ya mechi zijazo.

Taifa Leo imebaini kwamba mashabiki wengi hawaingii uwanjani kihalali ambapo shabiki ananunua tiketi moja na kuipiga chapa na kisha baadaye kuwauzia mashabiki wengine kwa bei ya juu, tiketi zote zikiwa zinafanana.

Yule ambaye atabahatika kuwa wa kwanza kuitumia tiketi hiyo iliyopigwa chapa, atafaulu kuingia. Waliosalia wote walionunua hufungiwa nje lakini baadaye wanatumia ujanja kuingia uwanjani.

“Ikiwa mashabiki hawatafuata sheria Jumapili, kuna uwezekano Kenya ikakosa kuandaa mechi ya robo fainali. Hii itakuwa ni hasara kwetu sote kwa sababu huo ni mchuano mkubwa. Hata huenda ikaathiri michuano ijayo ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027,” alisema Musonye jana wakati wa kikao na wanahabari Uwanjani Nyayo jijini Nairobi.

Aidha, ilibainika kuwa baadhi ya Wakenya walinunua tiketi kutoka kwa tovuti feki ambayo si halali ya chan.mookh.com. Ilibainika kuwa tovuti hii iliundwa na mkora aliyewatapeli Wakenya.