Habari za Kaunti

Diwani ashtua wakazi kwa kukata utepe na kuzindua masufuria kama zawadi

Na LUCY MKANYIKA  August 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWAKILISHI wa Wundanyi, Kaunti ya Taita Taveta, Bw Jimmy Mwamidi, aliwashangaza wakazi kwa kuzindua sufuria kama sehemu ya mpango wa kuviwezesha vijiji vya eneo hilo.

Hafla hiyo ya uzinduzi ilifanyika baada ya mwakilishi huyo kukata utepe uliokuwa umefungwa sufuria mbili huku viongozi na wanakijiji wa Mranju wakishuhudia kwa shangwe na nderemo.

Bw Mwamidi aliongoza hafla hiyo kwa kuwasihi wenyeji kuzitumia kwa shughuli za kijamii kama vile kupika katika mikutano na harusi za kijiji.

Katika tukio hilo lililozua hisia mseto miongoni mwa wakazi wa kaunti hiyo, Bw Mwamidi vilevile alitoa viti na vyombo vya plastiki, mitungi ya kuoshea mikono, birika na hema katika vijiji tano vya wadi hiyo.

Kama njia ya kuwezesha wakazi hao kupitia mpango wa serikali ya kaunti ya uwezeshaji wa jamii, Bw Mwamidi alisema kuwa uwekezaji huo utasaidia vijiji ivyo kuokoa pesa za kukodisha vifaa hivyo wanapovihitaji.

“Rasilimali zaidi zitabaki ndani ya jamii, na hivyo wataweza kujitegemea kwa muda mrefu,” alisema.

Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa kaunti ya Taita Taveta kuzindua vifaa kama hivyo kama sehemu ya mpango wa maendeleo.

Katika serikali ya sasa na zile zilizopita, kaunti hiyo, kupitia hazina ya wadi, imekuwa ikitenga mamilioni ya fedha ili kutoa vifaa vya aina hiyo kwa makundi ya jamii za kaunti hiyo.

Vifaa hivyo hutolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na mashirika ya kijamii kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.

Baadhi ya vifaa ambavyo hutolewa ni mahema, vipaza sauti, viti, sahani za plastiki, kuandaa mashindano ya mpira wa miguu na fedha kwa vyama vya wanawake na vijana.

Katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha, serikali ya kaunti imetenga zaidi ya Sh115 milioni kwa mpango huu wa uwezeshaji.

Huku baadhi ya vikundi vikifurahia misaada hiyo kama ishara ya kutambuliwa, wengine wanahisi kuwa ni dalili ya kushindwa kwa serikali ya kaunti kutekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi na kijamii.

Licha ya nia ya mpango huu kuwa njema, baadhi ya wakazi wamehoji iwapo vifaa kama hivyo vinaweza kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya wananchi.

Bi Isabella Kidede, mwanaharakati wa maswala ya bajeti alisema kuwa viongozi wanatumia hazina hiyo kujipatia umaarufu kisiasa badala ya kushughulikia matatizo ya msingi.

“Lazima tujiulize kuwa serikali ya kaunti inatathmini vipi ufanisi wa mipango hii? Ni kweli inawawezesha jamii, au tunatafuta makofi ya muda mfupi tu? Ikiwa uwezeshaji wa jamii ni ugavi wa sufuria, viti vya plastiki, na mahema, ni lazima tutafakari iwapo tumepoteza maana halisi ya uwezeshaji wa kweli au vipi. Vitu hivi havina uwezo wa kubadilisha maisha ya watu au kushughulikia umasikini na ukosefu wa ajira,” alisema.

Bi Kidede alisema kuwa mipango ya uwezeshaji inapaswa kuwa endelevu, na inayolenga mahitaji halisi ya wananchi.

“Inafaa kubadilisha maisha na kuinua jamii nzima ili iweze kujitegemea. Serikali ya kaunti inafaa kufikiria kuhusu mbinu inayotumia kwa sasa,” alisema.

Alisema licha ya madai ya viongozi na maafisa wa kaunti kuwa wananchi walipendekeza kupewa vifaa hivyo, ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wakazi wanatoa mapendekezo ya kuwanufaisha wakati yanapohitajika.

Aidha, aliwataka wananchi kusukuma uwajibikaji kutoka kwa viongozi.

“Jamii zetu zinastahili uwezeshaji unaolenga kuwapa matumaini, heshima, na fursa zaidi za kujiendeleza kimaisha. Viongozi wanafaa kuwaelekeza wananchi kwa njia inayofaa. Tusiwache wananchi watoe maoni kama haya bila kuwaelekeza vizuri,” alisema.