MAONI: Hivi tunawezeshwa na serikali ama imetuweza?
MIKUTANO ya kuwezesha makundi mbalimbali ya jamii kama vile wanawake na vijana imekuwa mingi kupita kiasi, ikisukumwa na serikali.
Mikutano hii imegeuka kuwa fursa ya Kenya Kwanza na washirika wake kuitumia kumwombea Rais Ruto muhula wa pili katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Ni majumuiko ambayo yamevunja kanuni za katiba.
Kwa mfano, Spika wa Bunge, Moses Wetang’ula, ambaye anatakiwa kuwa huru, amekuwa akizunguka kila mahali kuwashawishi watu waunge mkono Serikali Jumuishi na kuwataka wamtazame Rais Ruto kwa jicho la huruma kipenga kitakapolia.
Si yeye tu; Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, amekuwa mwanasiasa mahiri katika mikutano hii ya uwezeshaji, akiona masuala ya vijijini kuwa muhimu zaidi kuliko mambo ya nje.
Kamanda wa kikosi hicho ni Naibu Rais, Prof Kithure Kindiki.
Hata upinzani nao, baada ya kukashifu serikali, walifanya mkutano wa aina hiyo katika eneo bunge la Saboti.
Hapa ndipo ninaposhindwa kutofautisha malengo ya makundi haya mawili.
Suala hili limeshajadiliwa na Jaji Mkuu mstaafu, David Kenani Maraga, ambaye ameibua maswali mengi ya msingi.
Hizi hela zinazotolewa kwa makundi haya zinatoka wapi?
Tukitumia busara ya kiitikadi, kwa mfano, mshahara wa Spika ni milioni moja, lakini unampata ametoa karibu shilingi milioni tatu.
Je, hizo fedha za ziada zinatoka wapi? Ama ni mkarimu sana kiasi cha kutoa mali yake binafsi?
Pili, ikiwa lengo ni kuwezesha jamii, mbona ni makundi maalum pekee yanayofaidi kwa fedha hizo? Na tatu, ambayo ni muhimu sana: Je, mpango huu ni endelevu?
Kadhalika, wapo wanaouliza ikiwa mpango huu unaweza kutenganishwa na siasa za uchaguzi mkuu wa 2027.
Hoja ya uchaguzi mkuu ujao ndiyo inayowafanya wengi kudhania kuwa matukio haya si ya kihisani ama kuboresha maisha ya umma kwa upana.
Hili ni jambo kubwa ambalo, hata kabla ya kuanzishwa, lingehitaji ushirikishwaji wa umma ili kutoa ramani kamili ya jinsi ya kuendesha mpango huo.
Ikiwa hivyo ingefanyika, huenda mradi huo usingepigwa vita jinsi ilivyo sasa.
Michango inatofautiana kulingana na wageni mashuhuri wanaohudhuria hafla hizo, na hata mgao kwa walengwa si sawa licha ya baadhi ya makundi kuwa na malengo sawa.
Baadhi ya makundi tayari yameripoti kuwa fedha hizo zimeliwa na wachache, huku wengine wakilalamika kuwa walipokea kiasi kidogo, baadhi chini ya shilingi elfu moja kwa kila mshiriki.
Ni hadithi nyingi za manung’uniko kuliko za manufaa kutoka katika vikao hivyo.
Inawezekana washiriki wakaishia kutengana baada ya kugawana fedha hizo kuliko walivyokuwa kabla ya kuanza kwa mpango huo. Kuna kazi kubwa bado ya kuwawezesha wananchi wa Kenya.
Paul Nabiswa ni mhariri, NTV