Kifaa kinachosaidia kujua hali ya ndama kabla ya kuzaliwa
KUNA njia nyingi ambazo mkulima anaweza kutumia, kubaini ikiwa ng’ombe wake ametungishwa mimba au la.
Kuna mbinu ambazo zimetumika kwa muda kama kuangazia ikiwa ameongeza unene au mabadiliko ya umbo pamoja na mabadiliko ya tabia za mifugo wake.
Hata hivyo, wataalam wanaeleza kuwa utaratibu wa aina hii sio sahihi.
Sekta ya nyama na maziwa nchini huchangia kwenye kipato cha taifa ingawa kiwango cha uzalishaji hakitoshelezi mahitaji ya soko humu nchini na kimataifa.
Hali hii inaashiria kwamba bado kuna fursa nyingi za ajira kuanzia hatua ya kuboresha spishi za mifugo, malisho na mbinu bora za utafutaji wa soko.
Ni hali ambayo wataalam wanasema kuwa haitafaulu ikiwa wakulima wataendelea kushikilia matumizi ya nyenzo za kiasili, ambazo aghalabu hutumika vijijini miongoni mwa wakulima wenye kipato kidogo kwa sababu ya ukosefu wa zana za kisasa.
Bi Everlyne Akinyi mtaalam wa mifugo kutoka Kituo cha Beef Research Institute eneo la Lanet, Kaunti ya Nakuru, anasema mabadiliko ya sayansi yamefanya shughuli za kuweka data za mifugo kuwa nyepesi.
Kwa kutumia zana za kisasa, mkulima anaweza kutambua jinsia ya ndama na hatimaye kutoa maelezo ya kina kuhusu uzani, jinsia, umri na afya.

“Na vilevile anaweza kubaini hatua ya ukuaji ili kufanya maandalizi ya mapema kwa kutoa makadirio sahihi ya bajeti ya ufugaji kwa siku zijazo,” anasema.
Anasema kuwa wataalam walivumbua mtambo wa kutoa tathmini ya afya ya ndama sio tu kufanya uchunguzi wa mifugo wangali tumboni bali pia kuwasaidia wakulima kuepuka hali ya dharura.
Kwa upande mwingine, anasema kifaa hiki hutoa sura kamili ya ndama ambaye anatarajiwa, jambo ambalo limekuwa likiwatatiza wakulima wengi mashambani.
Mtambo huu umekuwa ukitumika nchini kuanzia miaka ya 90 lengo kuu likiwa ni kutoa nafasi kwa Wizara ya Kilimo na washikadau husika kuweka mipangilio ya uzalishaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa.
“Pia kupata habari ya namna gani wanaweza kuwahudumia wakulima wa mifugo,” anaeleza.
Bara la Afrika ni miongoni mwa mataifa ambayo husafirisha idadi kubwa ya ng’ombe wa nyama kwenda Ulaya, Botswana ikiongoza katika biashara hiyo.
Chombo hiki kimeboreshwa na mkulima anaweza kupokea taarifa kwa kupata picha kamili ya ndama akiwa angali tumboni.
“Kwanza kabisa kwa kuangazia maswala muhimu na mahitaji ya ng’ombe ni muhimu kuangazia ubora wa chakula, ili kujenga mazingira faafu ya ukuaji wa ndama kwa ajili ya siku za baadaye, anasema.
Mtambo huu humsaidia mkulima kwa sababu anaweza kuchukua hatua ya kutafuta ushauri kutoka kwa wataalam wa lishe ya mifugo kwa kuzingatia kiwango na namna ya kulisha mifugo wake.
Mtambo huu hautumiki tu miongoni mwa madaktari wanaoangazia afya ya mifugo bali pia wakulima ambao wanafuga idadi kubwa ya mifugo kwa shughuli za kibiashara.
“Kutoka hapo mtaalam wa mifugo anaweza kuchukua data za mifugo wake hata kabla ya kuzaliwa na kuzinakili kwa ajili ya kuzishughulikia,” anaongeza.