Hofu mapato ‘karibu yote’ ya Kenya, mwandalizi wa CHAN, yatamezwa na faini
KENYA sasa imepigwa jumla ya aini ya Sh10.5 milioni tangu kipute cha Kombe la Afrika kwa Wachezaji Wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024) ianze mwezi huu, hali hii ikichochewa na mashabiki kukosa kuzingatia sheria za CAF.
Faini hiyo imetokana na mashabiki kutofuata kanuni zilizowekwa wakati wa ushindi wa 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) pamoja na sare ya 1-1 dhidi ya Angola iliyofuatia.
Pia Kenya ilijipata pabaya baada ya mashabiki kuvunja lango na kuingia uwanjani bila kununua tiketi, kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Morocco.
Kupitia barua ya CAF kwa Shirikisho la Soka Nchini Kenya italipa pesa hizo na ipo hatari ya kupokonywa mechi zijazo kwenye kipute hiki.
Faini ya juu zaidi ni Sh6.5 milioni ambazo Kenya imepigwa katika mchuano dhidi ya Morocco Jumapili iliyopita.
Faini nyingine ilikuwa ni Sh2.5 milioni katika mechi dhidi ya DR Congo na Sh1.5 milioni katika mtanange dhidi ya Angola.
“Nawaomba mashabiki wadumishe amani, wafike uwanjani wakiwa na tiketi na wajizuie kushiriki ghasia kwa sababu hatutaki ghadhabu zaidi katika kipute cha CAF,” akasema Mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya CHAN (LOC) Nicholas Musonye.
Haya yanakuja wakati ambapo Harambee Stars itafahamu iwapo imetinga fainali kabla ya mechi ya Zambia au la.
Hii ni kwa sababu Morocco itakuwa ikivaana na Zambia leo katika uwanja wa Nyayo kuanzia saa 11 jioni.
Mechi nyingine itakuwa katika uwanja wa Kasarani kati ya DR Congo na Angola.
Kenya inaongoza Kundi A kwa alama saba na imebaki na mechi moja.
Angola ina alama nne huku DR Congo na Morocco zikiwa na alama tatu kila moja kisha Zambia haijaambulia alama zozote.
Kenya itakuwa ikiomba mechi hizi zitoke sare ili iwe imetinga robo fainali hata kabla ya mechi ya Jumapili.
Iwapo Angola itaipiga DR Congo basi itakuwa imefikisha alama saba sawa na Kenya japo itategemea pia idadi ya mabao.
Kwa upande mwingine Kenya itakuwa vibaya zaidi iwapo Morocco itaishinda Zambia kwa mabao mengi kuelekea mchuano wao wa mwisho dhidi ya DR Congo mnamo Jumapili.