Habari

Wimbi la ghasia lazuka Embu biashara za mamilioni ya pesa zikichomwa

Na GEORGE MUNENE August 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imetuma kikosi maalum cha wapelelezi mjini Siakago, Kaunti ya Embu, kufuatia wingu la visa vya ghasia ambavyo vimesababisha mali yenye thamani ya mamilioni kuharibiwa na wakazi kadhaa kujeruhiwa.

Machafuko yalizuka wakati wafanyabiashara wa Meru na Embu walipokabiliana vikali mjini humo, Mbeere Kaskazini, kuhusu uhasama wa kibashara.

Kwenye ghasia hizo, majengo ya kibiashara, magari na mali nyingineyo iliteketezwa.

Taharuki ilitanda huku makundi hayo mawili hasimu yakipigana na kusitisha biashara kwa siku mbili katika mji ambao kwa kawaida huwa wenye shughuli nyingi.

Waziri wa Huduma za Umma, Geoffrey Ruku, alitangaza kuwa  makachero wanatazamiwa kuendesha uchunguzi wa kina kubaini ukweli kuhusu tukio hilo.

Mali iliyoharibiwa wakati ghasia zilipozuka Siakago, Embu. Picha|George Munene

Aliwahakikishia wakazi kwamba wahusika wote wa ghasia watawajibika akionya watumishi wa umma akiwemo maafisa wa polisi ambao huenda walihusika na tafrani hiyo.

“Hakuna atakayenusurika. Afisa yeyote atakayepatikana kuwa alisaidia au kupuuza maovu haya ataadhibiwa kikamilifu kisheria,” alisema Bw Ruku.

Alikashifu ufisadi uliokithiri katika idara ya polisi akielezea wasiwasi kuhusu madai kwamba maafisa waliitisha hongo, almaarufu kama “kalamu au kifaa cha kuandikia” kabla ya kusaidia wahasiriwa wa uhalifu.

Wafanyabiashara walisimulia hasara waliyopata kwenye ghasia hizo na kuwashutumu polisi kwa kukosa kuwalinda.

Mfanyabiashara Peter Mutiru ambaye duka lake ni miongoni mwa zilizoharibiwa, alidai kamera za CCTV zilionyesha maafisa wa polisi wakiwalinda washambulizi.

“Nilipoteza takriban Sh5 milioni katika mashambulizi hayo na sasa ninateseka,” alisema.

Gari lililochomwa wakati ghasia zilipozuka mjini Siakago, Embu. Picha|George Munene

Wakazi wengineo walielezea masaibu yao kuhusu wafanyabiashara wakora wa muguka waliodaiwa kutoweka bila kulipia bidhaa zao na kuzidisha zaidi hasara ya kifedha iliyotokana na mashambulizi.

Wafanyabiashara wa Meru wamekuwa wakiendesha biashara zao mjini humo na wakazi wamewashutumu kwa kuchukua biashara zao ikiwemo za Muguka.

Baadhi ya wafanyabiashara Wameru walifurushwa katika mashambulizi hayo na kulazimika kutorokea mitaa mingineyo ya Embu.

Gavana wa Meru Mutuma M’Ethingia amekashifu shambulizi hilo akisema Wameru ni watu wanaojituma na wana haki kikatiba kufanya biashara, kumiliki mali, na kuishi sehemu yoyote nchini pasipo kuingiliwa.