Jamvi La Siasa

KINAYA: Hivi tunahitaji serikali za kaunti au tuzifunge ghafla kama vibanda vya mboga

Na DOUGLAS MUTUA August 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HIVI tunahitaji serikali za kaunti au tuzifunge ghafla kama vibanda vya kuuzia mboga-mboga, magavana watafute kazi nyingine?

Usinitukane wala kunitishia, hata Pasta Ng’ang’a wa Neno alitishia kufunga makanisa aliyoanzisha, akayaita vibanda, na hakuna kitu ulichomfanyia.

Nakuomba kwa muda unifananishe naye, useme nimetishia kufunga serikali za kaunti, halafu ukifanikiwa kutumia akili haraka ukumbuke sina uwezo wa kuzifunga.

Ni sawa na kuamka siku moja, nikwambie nitabadilisha Katiba ya nchi, halafu ukimbie kwa chifu wenu kunishtaki. Chifu anakuangalia na kujiuliza kati yangu nawe, kichaa ni nani.

Ghafla anaamua kutumia akili na kutanabahi kuwa kichaa ni wewe kwa maana nimekukoroga akili mpaka ukamkimbilia kumshtakia mambo ya kipuuzi yasiyowezekana kwa kauli ya mtu mmoja.

Ni siri iliyo wazi kwamba kusudio letu la kugatua mamlaka na rasilmali kutoka serikali ya Nairobi hadi mashinani lilituzalia matunda ambayo hatukutarajia.

Sijui unahisije, lakini binafsi sipendi kiburi cha serikali hizo ndogo, hasa baadhi ya magavana wanapojibeba kama marais wadogo, hali baadhi yao wanaongoza majimbo yaliyo na wanyamapori wengi kuliko watu.

Kikubwa zaidi kinachonikera ni ugatuzi wa ufisadi kutoka Nairobi na kuupeleka mashinani. Wezi wa mali ya umma wametapakaa kote nchini, ukijaribu kumshika huyu, mwenzake aliye mbali anapata nafasi ya kutoroka.

Zamani ungewanasa mafisadi kwa mtego mmoja kama panya au nzi, hata ukishindwa kuwafunga gerezani uwaogofye wengine waliokuwa na nia kama hiyo ikiwa wanatumia ubongo badala ya ukamasi.

Nyakati nyingine mimi hujiuliza iwapo kweli tunataka mabadiliko bora nchini, au tunatania tu. Kwa jumla, Mkenya ni mtu mwenye tabia mbovu sana.

Ikiwa una tabia mbovu, halafu upewe fursa ya kujichagulia kiongozi, si itakuwa rahisi sana kujichagulia aliye na tabia mbovu kama wewe?

Watu wanaovunja nyua na vizuizi vinginevyo ili waingie kwenye uwanja wa michezo na kutazama usakataji kabumbu bila kulipa ada za kiingilio hawana mamlaka yoyote ya kulalamika dhidi ya mafisadi.

Hicho ndicho kiwango cha ubora wetu, tusidanganye. Hata huo ugavana tungeupata leo, labda tungekuwa mafisadi wa kutupwa kuliko tulionao wakati huu. Ndizo sifa zetu hizo.

Ngoja usikie kiasi cha pesa kilichotumiwa wakati wa kongamano la magavana ambalo limefanyika Homa Bay juzi, ndipo utakapoanza kujiuliza kama mimi: Kwani Kenya hii inayoliwa bila kuisha ina pesa ngapi?

Utovu wetu wa nidhamu ndio chanzo cha matatizo ya nchi, kila wakati kudhani eti wizi ni kipaji, ukipewa wadhifa fulani ukose kuiba unaonekana mjinga wa mwisho.

Kenya itabadilika tutakapoacha kutamani kupata fursa za kula mali ya umma, kiasha tuwachague viongozi wasio na tamaa ya fisi.

mutua_muema@yahoo.com