Habari za Kaunti

Gavana wa Kericho Mutai alivyotimuliwa na wabunge wa Kaunti mara mbili ndani ya miezi 10

Na  VITALIS KIMUTAI August 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kutimuliwa kwa Gavana wa Kericho, Erick Mutai, kwa mara ya pili ndani ya miezi kumi na Bunge la Kaunti kumeibua tofauti kubwa za kisiasa kati ya serikali ya kaunti na bunge lake.

Kisa hiki pia kimeonyesha mgawanyiko mkubwa usiotatulika kati ya Dkt Mutai na naibu wake Fred Kirui kwa upande mmoja, na Spika wa Bunge la Kaunti, Dkt Patrick Mutai kwa upande mwingine.

Gavana huyo anatuhumiwa kusimamia serikali ambayo ililipa Sh85.7 milioni  kwa kampuni 46 kwa bidhaa na huduma ambazo hazikutolewa wala kazi kutekelezwa.

Juhudi nyingi za kuwapatanisha Dkt Mutai na Bw Kirui zimegonga mwamba kwa miaka mitatu iliyopita, huku maridhiano yao yakiendelea kwa muda mfupi tu kabla ya mzozo kuzuka tena zaidi ya mara tano.

Jumla ya madiwani 33 walipiga kura kumuondoa Dkt Mutai kupitia hoja iliyowasilishwa na Diwani wa Wadi ya Sigowet, Kiprotich Rogony, huku Gavana akiungwa mkono na madiwani 14 pekee.

“Inaonekana kwamba baada ya kuokoka kutimuliwa mwaka jana, Dkt Mutai alilegeza kamba, huku wapinzani wake wakifanya kazi kwa bidii kuhakikisha anang’olewa madarakani,” alisema Bw Peter Langat, kiongozi wa vijana na mkazi wa Kaunti ya Kericho.

Aliongeza: “Gavana alipaswa kuhakikisha anaungwa mkono na zaidi ya madiwani 20 kila wakati, akijua fika kuna nguvu kubwa ndani na nje ya kaunti zinazotaka kumtoa madarakani.”

Akizungumza na wanahabari baada ya kutimuliwa, Dkt Mutai alielekeza lawama kwa Spika wa Bunge la Kaunti, Dkt Patrick Mutai, akidai kwamba alitaka kumuondoa kwa hali na mali, na kwamba mfumo wa kupiga kura kwa njia ya kielektroniki ulivurugwa ili kutoa matokeo yaliyopangwa.

“Spika ana nia ya kumweka naibu wangu – Fred Kirui – kuwa Gavana, kisha naye amuondoe ili awe na nguvu na ushawishi katika eneo hili kabla ya uchaguzi mkuu ujao ambapo anapanga kugombea ugavana,” alidai Dkt Mutai.

Kuumizwa kwa diwani Alfred Kirui wa wadi ya Tebesonik, Bureti, kufuatia vurugu zilizozuka ndani ya bunge baada ya kura ya kumtimua gavana, ni ishara zaidi ya uhasama uliopo kati ya viongozi hao.

Bw Kirui alipoteza fahamu baada ya kushambuliwa na wenzake katika vurugu hizo, na alipelekwa kwa haraka nje ya ukumbi kabla ya kulazwa katika Hospitali ya Siloam.

Vita hivyo vilishuhudia madiwani – wa kiume na wa kike – wakishambuliana vikali, wengine nguo zao zikiraruliwa huku baadhi yao wakijipata sakafuni, wakilia, wakitukanana na kupiga mayowe.

Dkt Mutai alikabiliwa na mashtaka ya kutumia vibaya mamlaka, uteuzi wa maafisa wakuu kwa njia isiyo ya haki au kinyume cha sheria, na pia kuwatimua baadhi bila kufuata taratibu. Alishtakiwa kwa kuhusika na upotevu wa rasilimali za umma, kulipa wakandarasi mara mbili, kuvunja Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, Katiba, na Sheria ya Serikali za Kaunti.

Pia alidaiwa kutangaza nafasi za ajira kwa wahudumu wa afya na walimu wa elimu ya awali (ECD) ilhali kaunti haina uwezo wa kuajiri, hatua ambayo ilionekana kama mbinu ya kujipendekeza kwa wapiga kura.