Habari za Kitaifa

Maswali sita nyeti ya wabunge kwa IEBC

Na  SAMWEL OWINO August 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Kamati ya Bunge la Kitaifa imeorodhesha maswali sita makuu ambayo inataka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujibu huku maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 yakiendelea.

Kamati ya Uangalizi wa Utekelezaji wa Katiba (CIOC) imepanga kukutana na makamishna wapya wa IEBC wiki ya mwisho ya mwezi huu. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Caroli Omondi, alisema mkutano huo ni sehemu ya wajibu wa kamati katika kufuatilia utekelezaji wa Katiba na kuzuia mapungufu ya dakika ya mwisho katika maandalizi ya uchaguzi.

“Tunahitaji IEBC iendeshe uchaguzi wa kuaminika, na mkutano huu ni hatua kuelekea hilo. Tulikuwa tumepanga kukutana mapema.Sasa tumeamua kukutana wiki ya mwisho ya mwezi huu,” Bw Omondi aliambia Taifa Leo.

Kipaumbele cha kwanza katika ajenda ya wabunge ni jinsi IEBC inapanga kushughulikia zoezi la  mipaka ya maeneo ya uchaguzi ambalo halijatekelezwa kama inavyohitajika kisheria. Bw Omondi alionya kuwa kushindwa kukamilisha zoezi hilo kunaweza kuiweka IEBC kwenye hatari ya changamoto za kisheria kuhusu matokeo ya uchaguzi wa 2027.

Wakati wa mafunzo ya makamishna wapya jijini Mombasa mwezi uliopita, IEBC ilikiri kuchelewa kwa zoezi hilo, ambalo lilipaswa kukamilika kufikia Machi 2024. Mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Erastus Ethekon, alisema wameomba ushauri wa Mahakama ya Juu baada ya kushauriana na Mwanasheria Mkuu, na kwamba watahusisha wadau baada ya uamuzi wa mahakama kutolewa.

Wabunge pia wanataka maelezo wazi kuhusu lini usajili wa wapigakura utaanza na jinsi tume inavyopanga kusafisha sajili ya wapigakura, baada ya shughuli hizo kusimamishwa tangu uchaguzi wa 2022 kwa sababu ya ukosefu wa makamishna.

“Hii ni hatua muhimu ambayo vijana wengi wanaisubiri kwa hamu. Tume inapaswa kutoa tarehe rasmi,” Bw Omondi alisisitiza.

Wakati wa kikao jijini Mombasa, Bw Ethekon alitangaza kuwa usajili wa wapigakura utaanza Agosti 5, kufuatia shinikizo kutoka kwa vijana na viongozi wa kisiasa. “Sajili safi ya wapigakura ni msingi wa uchaguzi huru na wa haki,” alisema.

Swali gumu zaidi linalowahusu makamishna wapya ni watatekelezaje uamuzi wa Mahakama ya Juu wa kufutilia mbali uchaguzi wa urais wa 2017?

Mahakama hiyo ilisema kuwa kulikuwa na kasoro katika upeperushaji wa matokeo na dosari katika fomu zilizotumika kutangaza matokeo, jambo lililofanya IEBC ionekane kushindwa kutekeleza uchaguzi kwa viwango vinavyotakiwa na Katiba. Mahakama ilionya kuwa chaguzi zijazo zitakumbwa na changamoto hizo hizo ikiwa matatizo ya msingi hayatatatuliwa.

Bw Omondi alisisitiza kuwa kamati yake inataka kuona hatua madhubuti zikichukuliwa. “Uchaguzi ulifutiliwa mbali si kwa sababu ya idadi ya kura, bali kwa sababu ya mchakato mzima. Mahakama imesema bayana jinsi uchaguzi wa kuaminika unavyopaswa kuwa,” alisema.

Kamati pia imeeleza wasiwasi kuhusu dhana ya kuwa baadhi ya makamishna wapya waliteuliwa kwa upendeleo wa kisiasa. Bw Omondi alisema IEBC inapaswa kuchukua hatua za kurejesha imani ya umma.

Wakati wa kuwahoji mwezi Mei, Bunge lilipokea kiapo cha maandishi kutoka kwa watu watatu waliopinga uteuzi wa baadhi ya majina, yakiwemo ya Bw Ethekon, ambaye alihusishwa na Naibu Mkuu wa Wafanyakazi wa Ikulu, Bw Josephat Nanok  aliyemwajiri alipokuwa Gavana wa Turkana.

Pingamizi pia zilitolewa dhidi ya Bi Mary Karen Sorobit, ambaye aliwahi kuwa afisa wa Chama cha Jubilee, na Bw Hassan Noor Hassan, ambaye jina lake liliingizwa nje ya utaratibu rasmi.

Hata hivyo, Bunge lilikataa pingamizi hizo na kuwaidhinisha wote saba, likisema walitimiza matakwa ya Katiba kuhusu uwiano wa kikanda, kijinsia, ujuzi wa kitaalamu, na uzoefu katika usimamizi wa uchaguzi.

Swali lingine muhimu ni kuhusu bajeti ya uchaguzi ujao. Mapema mwaka huu, Naibu Katibu wa IEBC, Bw Obadiah Keitany, aliambia wabunge kuwa tume hiyo inahitaji Sh61.7 bilioni  kwa maandalizi ya uchaguzi wa 2027.

Fedha hizo zitagawanywa kwa miaka mitatu ya kifedha: Sh15.3 bilioni kwa mwaka wa 2025/26 kwa maandalizi ya kabla ya uchaguzi, Sh25.4 bilioni mwaka wa 2026/27, na Sh21 bilioni mwaka wa 2027/28.

IEBC pia inapanga kusajili wapigakura wapya milioni 5.7, hasa vijana, na kuongeza vituo vya kupigia kura kutoka 46,229 mwaka 2022 hadi 55,393. Tume inapanga kununua vifaa vipya vya teknolojia ya uchaguzi kwa Sh7 bilioni ili kuchukua nafasi ya vile vya 2017. Ni vifaa 14,000 tu vilivyonunuliwa mwaka 2022 vitakavyobaki kutumika.

“Vifaa vya zamani vimetumika kwa miaka 10. Tunaweza kuvitumia katika taasisi nyingine za serikali. Teknolojia imebadilika, nasi lazima tuende sambamba,” alisema Bw Keitany.

Teknolojia imekuwa sehemu kuu ya uchaguzi nchini Kenya tangu 2013 ilipoanza kutumika kurekebisha dosari zilizochangia machafuko ya baada ya uchaguzi wa 2007/08. Sheria ya Uchaguzi inaitaka IEBC kununua teknolojia hiyo angalau siku 120 kabla ya uchaguzi, na kuifanyia majaribio siku 60 kabla ya siku ya kupiga kura.