Makala

Njonjo alivyofuta usajili wa Gema aliyounga awali

Na BENSON MATHEKA August 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KATIKA kipindi cha miaka 17 alichohudumu kama Mwanasheria Mkuu, Charles Njonjo aliwashangaza Wakenya mara kwa mara kwa kutoa maoni yaliyokuwa kinyume kabisa na sera za nchi kuhusu masuala ya nje, au hata zile za Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) bila kujali hisia za wananchi.

Kwa mfano, alizua gumzo kwa kuunga mkono utawala wa wazungu uliokuwa wakati huo Afrika Kusini, ulioendeleza ubaguzi wa rangi, Rhodesia (ambayo kwa sasa ni Zimbabwe) na Msumbiji. Alitaka Kenya iendelee kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa ubaguzi Afrika Kusini jambo lililomkera sana Waziri wa Masuala ya Kigeni wakati huo, Dkt Munyua Waiyaki.

Njonjo pia alihusika katika mazungumzo kuhusu uvamizi wa kijeshi wa Israeli katika uwanja wa ndege wa Entebbe, Uganda, kuokoa mateka wa Kiyahudi waliokuwa wametekwa na magaidi katika ndege.

Aidha, alipinga vikali uwepo wa kikundi cha kikabila kilichoitwa Gikuyu, Embu and Meru Association (GEMA), ambacho yeye mwenyewe alikuwa amekisajili mwaka wa 1971 na baadaye, mwaka wa 1976, akataka kifutwe.

Njonjo alikuwa mtu wa karibu sana na Rais Jomo Kenyatta, kiasi cha kuwa mshauri wake wa kuaminika, hali iliyomfanya kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa sana serikalini. Ukaribu huo ulimfanya kuhusishwa na uteuzi wa Daniel arap Moi kuwa Makamu wa Rais wa tatu wa Kenya baada ya kujiuzulu kwa Joseph Murumbi, pendekezo ambalo Kenyatta alilipokea vyema.

“Tulipokuwa tukisafiri kwa gari la kifahari la rais kutoka mji mmoja Bonde la Ufa, baada ya Murumbi kujiuzulu, Mzee alijiuliza kwa sauti ni nani angemteua kuchukua nafasi hiyo. Kisha akaniuliza: ‘Unafikiri ni nani?’ Nikamjibu, ‘Unaonaje Moi?’” Njonjo alikumbuka.

Kwa mujibu wake, Kenyatta alipendezwa sana na wazo hilo kiasi cha kumteua Moi kuwa Makamu wa Rais siku iliyofuata.Kwa heshima yake, Njonjo alitunga sheria nyingi zilizoifanya Kenya kutoka kuwa koloni hadi kuwa taifa huru, na kuweka misingi ya taasisi ambazo ziliimarisha demokrasia na utawala bora chini ya uongozi wa miaka 15 wa Kenyatta.Alifunga ndoa mwaka wa 1972 akiwa na umri wa miaka 52. “Nilikuwa nimeolewa na kazi yangu,” alikiri.

Aliongeza, “Nilipenda kazi yangu ya Mwanasheria Mkuu, nilifanya kazi kwa saa zisizo za kawaida ambazo zingeweza kumkera mke. Kwa muda mrefu sikufikiria kuoa. Nje ya ofisi nilikuwa na burudani nyingi nilizofurahia sana na nilidhani hilo lilitosha.”Hata hivyo, alipata shinikizo kutoka kila upande. Kenyatta alijiuliza ni kwa muda gani angeendelea kushauriwa na mtu asiye na familia.

Mama yake Njonjo, Bi Wairimu, alitamani kuwa na wajukuu. Akiwa muumini wa Kanisa la Anglikana (ACK), ni kanisa ndilo lililomsaidia kupata mchumba. Mapema miaka ya 1970, wakati wa ibada katika Kanisa la All Saints Cathedral jijini Nairobi, alimuona msichana mmoja aliyekuwa akiimba katika kwaya.

Mara nyingine wangeketi kwenye kiti kimoja.“Ningemtazama nakujiambia, ‘Huyu ni msichana mzuri.’ Mchungaji wangu pia alidhani yeye ndiye angefaa kuwa mke wangu na alitualika, pamoja na waumini wengine, kwa chakula cha jioni nyumbani kwake,” Njonjo alikumbuka.

Margaret Bryson, raia wa Uingereza, alifahamiana vyema na Njonjo, na hatimaye walifunga ndoa katika harusi ya kukata na shoka Novemba 20 1972. Walijaliwa watoto wawili: msichana Wairimu na mvulana David.

Akiwa Mwanasheria Mkuu na baadaye Waziri, Njonjo alikuwa mfuasi mkakamavu wa sheria, jambo lililomfanya kusimama imara katika suala la urithi wa Kenyatta, akisisitiza kuwa lazima nchi ifuate utaratibu wa kikatiba.

Katiba ilieleza kwamba iwapo Rais aliye madarakani akifariki au kushindwa kuendelea kuhudumu, Makamu wa Rais angechukua nafasi kwa muda wa siku 90 kabla ya uchaguzi mpya kuitishwa.

Mwaka wa 1976, afya ya Mzee Kenyatta ilipoanza kudorora, Mwanasheria Mkuu alijitokeza kupinga vikali kampeni ya kikundi cha wanasiasa waliokuwa na msimamo mkali, wakiwemo wanasiasa wa Kiambu – Njoroge Mungai na Njenga Karume – pamoja na Kihika Kimani kutoka Nakuru, Harvester Angaine (aliyeitwa ‘Mfalme wa Meru’) na Paul Ngei kutoka Ukambani.

Lengo lao lilikuwa kubadilisha Katiba ili kumzuia Moi kutwaa urais moja kwa moja iwapo Kenyatta angefariki.Kampeni hiyo ya ‘Badilisha Katiba’ ilifikia kilele chake katika mkutano wa hadhara mjini Nakuru ambapo Paul Ngei alitoa kauli tata akiomba Wakenya wampe madaraka kwa siku tatu tu, na akaahidi kwamba asingeachilia uongozi tena.

Njonjo, ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa Moi, alipinga vikali mapendekezo hayo katika mjadala mkali Bungeni na kuwashtumu waliotoa pendekezo hilo kwa kuwazia kifo cha Rais – jambo ambalo alisema ni uhaini.Mpango huo ulizimwa kabisa kwa nguvu ya pamoja kati ya Moi, wafuasi wake na viongozi wengine kama Waziri wa Fedha, Mwai Kibaki, pamoja na Njonjo ambaye inawezekana alikuwa na maslahi ya kibinafsi ya kisiasa.