Mtoto anahitaji msingi thabiti katika malezi dijitali
KULEA watoto kunahitaji zaidi ya kuhakikisha wako usalama, wanakula, wanavaa na wanapata elimu.
Katika mazingira ya kisasa ya kidijitali, malezi yanahitaji maandalizi ya kina kuwasaidia watoto kuishi maisha yenye afya, si tu mitandaoni bali pia katika maisha halisi.
Watoto wa leo wanahitaji kujifunza si tu jinsi ya kuepuka hatari za mtandaoni na nje ya mtandao, bali pia kuwa na stadi mbalimbali zitakazowasaidia kustawi katika pande zote mbili.Kwa wazazi wengi, hasa kizazi cha milenia, hali hii ni changamoto, kwani wanalea watoto katika ulimwengu tofauti na ule waliokulia.
Ni vigumu kuelewa teknolojia wanayokutana nayo watoto wao, na hali hiyo ya kuchanganyikiwa ni ya kueleweka.Kwa bahati nzuri, watafiti wameanza kuchunguza dhana ya “malezi ya kidijitali” na kubaini mbinu bora zitakazosaidia watoto kustawi mtandaoni na nje ya mtandao. Siri sio tu kuweka mipaka au vikwazo.
Utafiti unaonyesha kuwa wazazi kuzungumza na watoto kuhusu matumizi ya mitandao na kuwapa mwongozo hupunguza hatari ya madhara ya mitandao ya kijamii na pia dalili za msongo wa mawazo.
Hata hivyo, utafiti mpya unapendekeza kwamba pamoja na mzazi kuwekea watoto sheria, mipaka na ufuatiliaji huenda ndio njia bora zaidi ya malezi ya kidijitali.
Watafiti wanasema wazazi wanaoweka mipaka na pia kusaidia watoto wao huripoti dalili chache za matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kuliko wale wanaoweka mipaka lakini hawafuatilii.
Wanasema hii ni muhimu zaidi katika kuzuia matumizi hatari ya mitandao. Watafiti waligundua kuwa vijana huwa na uwezekano mkubwa wa kuheshimu sheria iwapo wanapata mapenzi na msaada kutoka kwa wazazi wao.
“Kumbuka, sheria na mipaka ni ya muhimu, lakini mazingira ya nyumbani ndiyo hutoa ulinzi wa kweli kabla mtoto hajafikia kifaa chochote cha kidijitali. Uhusiano wa karibu huwasaidia watoto kutotumia mitandao ya kijamii kujaza pengo la mahitaji ya kisaikolojia yasiyotimizwa,” asema mtaalamu wa malezi dijitali Suzanne Geurts.
Utafiti huu unaunga mkono wazo kwamba maisha ya nje ya mtandao ya mtoto yana athari kubwa kwa jinsi wanavyokabiliana na changamoto za mtandaoni.Wazazi wakijenga mazingira salama, yenye upendo, mazungumzo ya kina, na kuweka mipaka ya kidijitali, watoto watakuwa na uwezekano mdogo wa kuingia kwenye tabia hatari.